NAIBU Rais wa Kenya Rigathi Gachagua alikiri Jumapili, Aprili 9, 2023, kwamba baadhi ya watumishi na viongozi wakuu wa taasisi za umma walikuwa bado hawajapokea mishahara yao ya Machi huku kukiwa na ripoti za uhaba wa pesa.
Akizungumza wakati wa ibada katika kanisa la PCEA Ngorano Centre eneo la Mathira kaunti ya Nyeri, kiongozi huyo wa pili nchini humo alihusisha kucheleweshwa kwa mishahara hiyo na ukomavu wa madeni ambayo ulipaji wake ulipewa kipaumbele na serikali.
Gachagua alilaumu utawala uliopita wa Uhuru Kenyatta na nduguye Raila Odinga kwa “kuharibu uchumi wa nchi” kwa uchu mkubwa wa mikopo.
“Ni kweli tuna changamoto katika kulipa mishahara na kutoa pesa kwa magavana kwa sababu serikali ya handshake iliharibu uchumi huu. Walikopa pesa kushoto, kulia na katikati,” Gachagua alisema.
“Kwa sababu sisi ni serikali inayowajibika, lazima tulipe pesa hizi.”
Chanzo: K24 TV