WANANCHI katika Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara wametakiwa kuunga mkono uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali kwa kuleta fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa mradi wa shule ya msingi Chawi iliyopo kwenye halmashauri hiyo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Stergomena Tax amesema serikali hiyo inaendelea kutatua kero zilizopo kwenye maeneo yao kwa kuwaletea maendeleo.
“Miradi mbalimbali inetekelezwa katika sekta mbalimbali kwenye maeneo yenu, kila mtu ana iona kazi inayofawa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika maeneo yenu”
Amesema serikali hiyo imedhamilia kuboresha maisha ya Watanzania kupitia miradi mbalimbali katika sekta zote ikiwemo miundombinu ya barabara, umeme, afya, uendelezaji wa viwanda, kuvutia uwekezaji na mingine.
SOMA: Madiwani Nanyamba wamshukia DED kupuuza hoja
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mhandisi Hashim Munde amesema ujenzi wa shule ya msingi Chawi ni wa madarasa saba ikiwemo wawili shule ya awali, jengo la utawala pamoja na vyoo uliyogharimu zaidi ya Sh milioni 300.
Aidha mradi huo una uwezo wa kuchukuwa wanafunzi zaidi ya 500 na ujenzi kwa sasa umeleta hamasa kwa jamii kuweza kupeleka watoto shuleni ikilinganishwa na hapo awali kabla ya ujenzi.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema kuna miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa katika mkoa huo ikiwemo bandari, uwanja wa ndege lakini pia huduma za kijamii kama vile hospitali, vituo vya afya na zingine.
Aidha, Waziri huyo wa Ulinzi bado anaendelea na ziara yake ya kikazi ya siku tano mkoani humo kwa ajili ajili ya kufungua na kuweka jiwe la msingi miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza wa wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara.