Nanyumbu wakamilisha barabara ya lami Mangaka

Nanyumbu wakamilisha barabara ya lami Mangaka

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Halmashauri ya Nanyumbu, mkoani Mtwara, imekamilisha ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.8 na kufunga taa 40 kwa kutumia fedha za tozo ya mafuta  (Fuel levy), shilingi bilioni moja, ambazo zilitolewa na serikali mwaka wa fedha 2021/22.

Barabara hiyo ni ya kwanza kujengwa katika mji huo wa Mangaka, Halmashauri ya Nanyumbu, toka uanzishwe mwaka 2007 na kuweka historia ya maendeleo ya mji huo kuwa na barabara ya lami.

“Mji wa Mangaka haujawahi kuwa na hata kilomita moja ya lami kwa maana ya upande wa barabara zinazosimamiwa na TARURA, hii ndiyo lami ya kwanza,” amesema Meneja wa TARURA Nanyumbu, Mhandisi Hussein Mwombeki.

Advertisement

Amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022, serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 2.4 na kati ya hizo Sh bilioni moja ikiwa ni za tozo ya mafuta, ambayo imetumika katika kujenga na kufunga taa 40 katika Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 1.8.

Mhandisi Mwombeki amesema barabara imejengwa katika sehemu ambayo inaenda hospitali, ofisi za serikali pamoja na huduma za kifedha.

“Watu walikuwa wanapata shida sana wanalalamika kila siku ,barabara kabla ya hapa ilikuwa na mashimo, mvua ikinyesha inakuwa ngumu kupitika,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mwombeki amesema kuwa wakala huo (TARURA), umejenga madaraja kumi na drifti mbili maeneo ya vijijini kwa kutumia fedha za jimbo shilingi milioni 500.

“Katika mwaka wa fedha 2021/2022 serikali ilitupatia kiasi cha shilingi bilioni 2.4 na katika hizo fedha zimegawanyika katika makundi matatu, fedha ya jimbo Sh milioni 500, bilioni moja tozo na milioni 780 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya barabara,” amesema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *