Nape azungumzia sheria kulinda taarifa binafsi mtandaoni

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Baraza la Mawaziri limeruhusu kutungwa kwa sheria itakayolinda taarifa binafsi katika mtandao.

Nape alisema hayo Jumatano Dar es Salaam kwenye ufunguzi wa kongamano la wadau wa teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) wakiwemo wa miundombinu wa ndani na nje ya nchi (Connect to Connect Tanzania).

Alisema ili mtandao uwe salama ni lazima kuwe na sheria na kwamba watachukua maoni ya wadau hao na kufanyiwa kazi yasaidie kuhakikisha taarifa za mtu binafsi zinalindwa kusaidia kupunguza changamoto zinazowakuta watu kwenye mitandao.

“Nataka kutoa wito kwa wote wanaohusika kutoa maoni yao na yatazingatiwa na sheria itapelekwa kusomwa Bunge lijalo Septemba 13, mwaka huu,” alisema Nape na kuongeza baada ya mchakato huo itatungwa sheria kwa kujifunza mapungufu kwa waliowatangulia itakayolinda taarifa za mtu binafsi.

Alisema wizara imejiandaa kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati sheria hiyo ikishapitishwa na ana uhakika Rais Samia Suluhu Hassan ataisaini na ianze kutumika mara moja.

Nape alisema serikali itahakikisha inaweka nguvu ili Tanzania iwe kitovu cha uchumi wa kidijiti kutokana na uwekezaji unaofanywa kupitia sera na mipango ya kimaendeleo.

Mkurugenzi wa masuala ya kisekta wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Emmanuel Manase alisema Mamlaka ya Mawasiliano na serikali inatengeneza mazingira wezeshi kwa wawekezaji kutoa huduma bora zinazomfikia Mtanzania kuhakikisha kila mtu anapata faida na huduma za mawasiliano.

“Kupitia mkutano huu tunaendelea kujifunza njia bora, salama na jinsi ambavyo ubunifu unaweza kutumika na kutupeleka hatua nyingine kama taifa na kuhakikisha hatubaki nyuma katika suala zima la kupata mawasiliano,” alisema.

Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia alisema wamefurahi kusikia taarifa za sheria itakayolinda taarifa binafsi kupelekwa bungeni itakuwa ni faida kwani hata wao walishapeleka maoni yao hawana shaka watazingatia.

Mworia alisema uwepo wa sheria utasaidia ubunifu kuwa na mazingira yenye tija kwa watoa huduma na walaji itawasaidia kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button