Nape: Mabadiliko ya Sheria ya Habari yaja

Nape Nnauye

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema serikali ina nia ya dhati kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Habari.

Nape aliwaeleza wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI) Dar es Salaam kuwa serikali imepokea maoni yao kuhusu marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari Na 12 ya 2016.

Kikao hicho ni cha pili cha wadau hao na serikali cha kupitia mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari, kiliongozwa na Nape mwenyewe.

Advertisement

“…tupo kwa ajili ya kufanya mapitio ya mwisho ya mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya 2016,” alisema Nape.

Nje ya kikao hicho, Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), alisema kuna mwelekeo mzuri kuelekea mabadiliko ya sheria ya habari.

‘‘Kikao kilikuwa kizuri, serikali imeendelea kuonesha dhamira yake ambayo ilikuwa nayo tangu mwanzo. Tumemaliza na serikali inaendelea na hatua zake kabla ya kupelekwa bungeni.

‘‘Suala la mabadiliko ya vipengele vya sheria lina mchakato wake, cha msingi serikali imetoa fursa, na si kutoa peke yake, inaendelea kuchukua hatua,’’ alisema Balile.

Miongoni mwa mapendekezo ya CoRI kwa serikali ni pamoja na mamlaka ya Mkurugenzi wa Habari (MAELEZO) yafutwe na kiundwe chombo ambacho pamoja na mambo mengine, kitashughulikia masuala ya usuluhishi yanapotolewa malalamiko dhidi ya chombo cha habari, badala ya kazi hiyo kufanywa na mtu mmoja.

Wadau wanataka marekebisho dhidi ya kifungu cha 6 (e) kinachoelekeza magazeti kupatiwa leseni badala ya usajili wa moja kwa moja.

Pia wadau hao wanapendekeza magazeti yasiendeshwe kwa kupewa leseni, badala yake yapewe usajili wa kudumu au wa muda mrefu, ili kudhibiti changamoto ya ufutwaji holela wa leseni na kuvutia wawekezaji.

Mapendekezo mengine kuhusu sheria hiyo, ni marekebisho dhidi ya kifungu chake cha 7 (2) (b) (lV), kinachoelekeza vyombo vya habari kutangaza au kuchapisha habari na masuala yenye umuhimu kwa taifa, kadiri itakavyelekezwa na serikali, wadai wakieleza kipengele hiki kinaingilia uhuru wa uhariri.

Sheria nyingine zinazolalamikiwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Huduma za Posta (EPOCA, 2010), Sheria ya Makosa Mtandaoni (2015), Sheria ya Haki ya Kupata Habari (2016) na Kanuni za Maudhui Mtandao (2018) kama zilivyorekebishwa mara kadhaa.

Wadau walioshiriki kikao nicho ni pamoja na TEF), Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Chama wa Waandishi wa Habari Tanzania (JOWUTA) na MISA- Tanzania.