Nape: Watanzania wanastahili huduma bora ya mawasiliano

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema serikali inafanyia kazi malalamiko yanayotolewa na wananchi kuhusu huduma za mawasiliano.

Nape alisema hayo Arusha wakati anafungua kikao kazi cha siku tatu cha viongozi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.

Alisema Watanzania wanastahili huduma bora na rahisi za mawasiliano zinazopatikana kila mahali.

Nape alisema mwaka huu Tanzania imeahidi kurusha satelaiti yake na kusisitiza wakati wowote satelaiti itarushwa.

“Tulipokwama, tuliposuasua tutafanya tathmini ya kina na kuambiana hali ilivyo ikiwamo kufanya maboresho ili mwaka huu wa fedha 2023/24 tuweze kuendelea mbele,” alisema.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa muda anaoutoa katika maboresho ya Wizara ya Habari sanjari na kuhudhuria shughuli zinazofanyika.

Nape alisema wizara imepitia sheria, sera na kanuni zinazosimamia mambo ya habari.

“Tulipofanikiwa ni vizuri kupongezana na tutaangalia tuliyojipangia mwaka huu wa fedha yapo mambo mbalimbali, lakini naamini tunaweza na tutafanikiwa, tushikamane zaidi,” alisema.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohamed Khamis Abdulla alisema wizara hiyo imepata mafanikio kwa sababu ya upendo, umoja na amani walionao viongozi na watumishi kwa ujumla.

Abdulla alihimiza viongozi wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo watumie nafasi zao za kimamlaka kwa kuwaelekeza kazi wafanyakazi wa chini ili nao wajitume zaidi.

“Watumishi tukiwa na umoja na kujituma ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu yetu na ninaomba tufanye kazi kwa kujituma na si kushurutishwa kwa sababu hakuna haki bila wajibu,” alisema.

Abdulla aliagiza wakuu wa taasisi wasimamie utekelezaji wa sera, kanuni, miongozo na taratibu zinazohusu haki na utawala bora na wasimamie stahiki za wafanyakazi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Shomari Omari Shomari alishukuru wizara hizo mbili za Zanzibar na Tanzania Bara kushirikiana na akaahidi kuimarisha ushirikiano huo.

Katika kikao hicho, mada mbalimbali zitatolewa zikiwamo mawasiliano ndani ya taasisi, Tanzania ya kidijiti, mabadiliko ya sera ya Tehama, mpango kazi wa shughuli za kazi, maadili ya utumishi wa umma, utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka sanjari na usalama na utunzaji wa siri za kikazi.

Habari Zifananazo

Back to top button