NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, ameihimiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) kuendelea kupanua wigo wake na kuwa mfano wa kuigwa na nchi za Afrika katika kukuza sekta ya uhasibu nchini.
Waziri Chande amesema hayo wakati akihutubia wahitimu 1,216 katika mahafali ya 46 ya NBAA yaliyofanyika Ukumbi wa APC Hotel, Bunju, jijini Dar es Salaam.
Aidha Waziri Chande alieleza kuwa idadi ya wahasibu wenye sifa nchini bado haitoshelezi mahitaji ya sekta ya umma, achilia mbali sekta binafsi na kusistizq kuwa NBAA ina jukumu la kuhakikisha wahitimu wake wanapata ujuzi wa hali ya juu ili waweze kuchangia kwa tija katika uchumi wa taifa.
SOMA: Washiriki mafunzo NBAA watakiwa kuboresha ufanisi
Amewataka wahitimu kuanzisha makampuni binafsi na kufuata taratibu za kisheria, huku akiweka ahadi kwa niaba ya Serikali kuunga mkono jitihada zao kwa kuandaa mazingira rafiki ya biashara.
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, ameelezea mchango mkubwa wa Wizara ya Fedha kwa Bodi, hususan katika kutoa ushauri wa kitaalamu. Amesema kuwa bodi imekuwa ikifanya mapitio ya sera na sheria zake, ambapo mwaka 2024 walitumia sheria ndogo tatu kusimamia mambo ya msingi, ikiwa ni pamoja na watu wanaoomba au kukata rufaa.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, ametangaza mpango wa kuanzisha stashahada maalum kwa njia ya mtandao ili kuongeza fursa za mafunzo kwa wataalam wa uhasibu nchini. Alisisitiza kuwa uadilifu ni msingi muhimu katika taaluma ya uhasibu, akiwataka wahitimu kusimamia maadili na kufichua maovu pale yanapojitokeza.
SOMA: NBAA watumia michezo kusaidia wagonjwa wa saratani
Kati ya wahitimu 1,216, wanawake walikuwa 640 na wanaume 576. Hafla hiyo ilihitimishwa kwa wito wa viongozi wa NBAA kwa wahitimu kuhakikisha wanaongeza thamani katika usimamizi wa rasilimali za taifa na kutoa ushauri mzuri unaojenga taifa.