NBAA yatoa elimu changamoto hati chafu

DAR ES SALAAM: Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) imetoa elimu ya kitaalamu kuhusu changamoto ya hati chafu zinazojitokeza kwenye baadhi ya Halmashauri na Taasisi mbalimbali nchini, ambapo imeeleza kuwa chanzo chake si wahasibu pekee kama ambavyo jamii imezoea kudhani.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Utafiti, Viwango na Uhasibu wa NBAA, CPA Angyelile Tende, amesema mara nyingi changamoto hizo huibuka kutokana na mambo tofauti ikiwemo upungufu wa taarifa sahihi za mapato na matumizi kwenye mashirika na taasisi zinazokaguliwa. Amesema hali hiyo huchangia upotoshaji wa taarifa za kifedha na kusababisha kasoro zinazojitokeza wakati wa ukaguzi.

CPA Tende ameongeza kuwa ni muhimu jamii kuelewa kuwa suala la hati chafu ni matokeo ya mfumo mzima wa usimamizi wa fedha katika taasisi husika, hivyo suluhisho lake linahitaji ushirikiano mpana badala ya kuwalaumu wahasibu pekee.

Aidha, amefafanua kuwa majukumu ya NBAA ni kusajili wanachama na wanafunzi, kutunga viwango vya uhasibu na ukaguzi, pamoja na kumshauri waziri mwenye dhamana ya masuala ya uhasibu na ukaguzi. Majukumu hayo yamekuwa yakitekelezwa tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo mwaka 1972, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Uhasibu na Ukaguzi.

SOMA ZAIDI

Ufaulu mitihani NBAA wapanda

Kwa upande wake, Mkuu wa Utafiti na Ushauri wa Kiufundi wa NBAA, Scola Mgimwa, amesema taasisi hiyo imekuwa ikiendesha mashindano ya uhasibu na ukaguzi kila mwaka kwa taasisi na mashirika mbalimbali nchini.

Amesema lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha ufanisi, uwajibikaji na matumizi bora ya viwango vya kitaaluma katika sekta ya uhasibu na ukaguzi.

Ameeleza kuwa kupitia mashindano hayo, taasisi hushindanishwa kwa kuzingatia namna zinavyotekeleza taratibu za kifedha na ukaguzi, hatua inayosaidia kuongeza ari ya ushindani wa kitaaluma na kuboresha taswira ya sekta ya uhasibu nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button