NBAA, ZIAAT kuzidisha ushirikiano

DAR ES SALAAM: BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri Elekezi Zanzibar (ZIAAT) wanatarajia kusaini mkataba wa ushirikiano unaolenga kubadilishana uzoefu na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Ushirikiano huo unalenga kuongeza ufanisi, uadilifu, na uzalendo ili kufikia malengo ya serikali ya uchumi endelevu.

Advertisement

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Kanuni Ndogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mihayo Juma N’Hunga, alitoa taarifa hiyo wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati hiyo, pamoja na viongozi wa ZIAAT, waliotembelea ofisi za NBAA ili kuimarisha ushirikiano na kuongeza tija katika sekta ya uhasibu.

“Mashirikiano hayo yatasaidia kuimarisha mahusiano kati ya Baraza la Wawakilishi, ZIAAT, na NBAA, ambapo taasisi hizi mbili zitabadilishana uzoefu ili kuongeza ufanisi wa kazi,” amesema Mihayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, ameongeza kuwa NBAA, ambayo ni mwanachama wa Shirikisho la Wahasibu Duniani (IFAC), imeendelea kusimamia viwango vya kitaaluma na kuendeleza wahasibu wanaoweza kufanya kazi kwa viwango vya kimataifa, hatua inayosaidia pia wahasibu kutoka Zanzibar kupitia ZIAAT kufikia viwango vya kimataifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZIAAT, CPA Ame Burhan Shadhil amesema kuwa taasisi hiyo changa imepata fursa ya kujifunza kutoka NBAA kuhusu usimamizi wa wanachama na maadili ya kitaaluma kwa lengo la kukuza utaalamu wa wahasibu Zanzibar.

SOMA: NBAA yatakiwa kuiga nchi zingine

Ziara hiyo pia imetoa fursa kwa Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi, kama alivyosema mjumbe Mwanaasha Khamis Juma, ambapo kamati imepata maarifa mapya ya kuboresha kanuni za uhasibu Zanzibar kwa ufanisi zaidi.

Mashirikiano haya yanatarajiwa kuleta mchango muhimu katika kufanikisha malengo ya serikali ya uchumi endelevu kwa kuwa na wahasibu wenye viwango vya kimataifa na maadili bora.