Nchi EAC ziimarishe umoja ajenda ya umeme

MKUTANO wa Wakuu wa Nchi wa Afrika Kuhusu Nishati unahitimishwa leo ukilenga kutoa azimio litakalowezesha Waafrika milioni 300 kufikishiwa huduma ya umeme ifikapo 2030.

Jana ulitanguliwa na mawaziri wa kisekta na leo wakuu wa nchi wanakaa kuhitimisha.

Pamoja na mambo mbalimbali yaliyojiri tangu jana, tunapongeza hatua ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
kutambua na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia Afrika.

Advertisement

Kwenye majadiliano katika siku ya kwanza ya mkutano, Rais wa AfDB pia amesifu juhudi za Serikali ya Tanzania za
kusambaza umeme katika vijiji vyote nchini.

Hili ni jambo la kujivunia kwa Tanzania na pia chachu kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inayoundwa na nchi
zilizoridhia kushirikiana katika nyanja mbalimbali.

Nazo ni; Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan Kusini na Somalia.

Akifungua mkutano huo jana, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema mwishoni mwa mwaka huu, Tanzania inatarajia uwezo wake wa uzalishaji umeme utafikia megawati 4,000 ambao asilimia 61 zinatoka katika vyanzo vya nishati safi.

Aidha, Tanzania imefikia vijiji 12,000 na katika ushirikiano na nchi nyingine, imeunganisha mtandao na nchi kama vile Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda. Pia njia nyingine za kuunganisha na nchi nyingine zinajengwa.

Kama alivyoshauri rais wa AfDB, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki awajibike na kutekeleza kwa vitendo ajenda ya nishati safi ili kuokoa wanawake na watoto dhidi ya madhara yatokanayo na nishati chafu.

Rai ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Biteko kuhusu kuwekeza kimkakati katika sekta ya nishati ili kufikia malengo yaliyokusudiwa, pia ichukuliwe kwa uzito.

Ukinara wa Tanzania kupitia kwa Rais Samia ni mwelekeo bora wa kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kikanda katika kuboresha upatikanaji wa nishati safi. Huu ni wakati muafaka kwa nchi wanachama wa EAC kuungana na kuibeba ajenda hii ya umeme kwa pamoja.

Kila nchi mwanachama itambue kwamba nishati safi ni nguzo muhimu katika maendeleo endelevu ya taifa lolote, ikichangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza umaskini, kuboresha afya na kukuza uchumi.

Ni wazi, kila moja ina mazingira na rasilimali tofauti zinazoweza kutumika katika uzalishaji wa nishati, hivyo
ushirikiano huu utasaidia kuboresha utoaji wa huduma hii muhimu.

Hivyo nchi nyingine, ziangalie mazingira na aina ya nishati inayoweza kuzalishwa kwa kuzingatia kwamba nishati safi si tu ni hitaji la kiuchumi, bali pia ni haki ya kimsingi kwa kila raia.

Kwa hiyo, ni wajibu wa viongozi wote wa EAC kuonesha dhamira yao katika kutimiza ndoto hii ya nishati safi kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Ni wakati sasa wa nchi wanachama wa EAC kuimarisha ushirikiano na kuchukua hatua madhubuti katika kuibeba ajenda ya umeme.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *