Ndege ya mizigo ATCL kusafirisha  chanjo DRC

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeamua kutumia ndege mpya ya kisasa ya mizigo Boeing 767-300 inayomilikiwa na Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), kusafirisha shehena ya chanjo zilizotoka India kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kupakia shehena hizo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), mmoja kati ya wadau wa usafirishaji mizigo wa anga, John Lupembe amesema sababu ya kutumia ndege hiyo ni kutokana na ubora wa huduma unaotolewa na ATCL,  pamoja na uwezo wa ndege hiyo kubeba bidhaa zenye mahitaji tofauti tofauti.

Lupembe amesema  kuwa  ndege hii imepunguza adha kubwa ya usafirishaji wa mizigo hapa nchini, ikiwemo bidhaa za aina ya chanjo ambazo huhitaji kiwango maalumu cha joto, ili kulinda ubora wake.

Advertisement

Kwa upande wa ATCL, Meneja Biashara Edward Nkwabi amesema wana uzoefu wa kutosha katika kusafirisha shehena za dawa na chanjo.

Ameeleza hapo awali, walikuwa wakitumia ndege yao ya masafa ya mbali ya abiria Boeing 787-8 Dreamliner kusafirisha mizigo ya aina hiyo.

Nkwabi amesema ATCL wataendelea kutoa Kipaumbele katika kuwezesha harakati za Mashirika ya Umoja wa Mataifa kama sehemu ya mchango, ili kufanikisha huduma za uokozi duniani.

Meneja huyo amesema wasafirishaji wa mizigo hawana budi kutumia fursa hiyo iliyoletwa na serikali katika kuhakikisha wafanyabiashara wa ndani ya nchi wanaendelea kunufaika.

“Nia ya ndege hii ilikuwa ni kuchochea bidhaa zetu za ndani kusafirishwa kwenda nje, hivyo tunahitaji ushirikiano wa Serikali kuhakikisha wanaongeza thamani ya bidhaa zao kwa kuwa zinaondokea hapa hapa,” amesema Nkwabi.

Amesema licha ya shirika hilo kuanza biashara ya usafirishaji na ushindani uliopo sokoni, bado ndege hiyo ya mizigo inatoa huduma kiasi cha kuendelea kuaminiwa na Mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF.

Naye, Mbarouk Mbarouk, rubani Mtanzania anayeongoza ndege hiyo, amesema leo wanakwenda Kinshasa na tani 26 za mzigo, pia watachukua mizigo mingine jijini Nairobi na kurudi Tanzania.

 

 

2 comments

Comments are closed.