Ndege ya mizigo kupenyeza bidhaa masoko makubwa

WAFANYABIASHARA wamesema ndege mpya ya mizigo aina ya Boeing 767-300F yenye uwezo wa kubeba tani 54 za mizigo iliyonunuliwa na serikali itasaidia bidhaa za Tanzania kupenya kwa urahisi kwenye masoko ya Ulaya, Asia na Amerika.

Wameyabainisha hayo walipozungumza na HabariLEO.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Stephen Chamle alisema wafanyabiashara wa Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto ya kusafirisha mizigo inayohitajika haraka kama maua, mbogamboga, matunda, samaki na nyama ambavyo vinapatikana kwa wingi hapa nchini.

Chamle alisema bidhaa hizo zimekuwa hazipenyi kwenye masoko makubwa ya dunia ikiwemo Ulaya, Asia na Amerika, hivyo ujio wa ndege hiyo utasaidia bidhaa hizo kufika kwenye masoko hayo kwa urahisi.

“Ujio wa ndege hii utatia chachu ya wafanyabiashara kuona fursa zilizopo nje, tuna bidhaa nyingi, kwa mfano Kanda ya Ziwa kuna samaki na nyama, kuna mikoa inazalisha matunda na mbogamboga kwa wingi, Arusha inazalisha maua kwa wingi, hivyo tuna uhitaji mkubwa wa ndege za mizigo,” alisema.

Pia alisema ili ndege hiyo iwanufaishe zaidi wafanyabiashara wa Tanzania, serikali haina budi kuboresha mifumo yake zikiwemo sheria ya uwekezaji, sheria inayosimamia biashara na sheria ya kodi.

Alisema kama mifumo hiyo haitakuwa rafiki kwa Watanzania, inaweza kuwa fursa kwa wafanyabiashara kutoka nchi nyingine kuja kununua maua, samaki, mbogamboga na kuitumia ndege hiyo kusafirisha kwenda nje kama Marekani kwani jambo hilo linawezekana.

“Tutengeneze mfumo ambao wenzetu huko nje huwa na sheria ya kuwalinda wenyeji, kuwalinda wananchi wake, siyo upendeleo lakini ni faida ambazo mgeni hapati, mgeni ana maslahi yake, mimi ni Mtanzania sina maslahi zaidi ya utanzania wangu,” alisema.

Meneja wa Mazingira ya Biashara wa Chama cha wakulima wa mbogamboga na matunda Tanzania (TAHA), Kelvin Remen alisema TAHA imekuwa ikiiomba serikali kuwekeza katika ndege ya mizigo kwa muda mrefu kwani walikuwa wakisafirisha bidhaa zao kwa kutumia ndege za abiria.

“Ndege hii itakuwa na mchango mkubwa katika kukuza tasnia ya kilimo cha mbogamboga na matunda hususani kama itakuwa inakwenda katika nchi zenye masoko muhimu kama Ulaya Magharibi, Mashariki ya Kati na Afrika Mashariki,” alisema na kuongeza:

“Masoko makubwa ya bidhaa za mbogamboga na matunda ni Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), India, Kenya na Uganda. Wastani wa mizigo ya bidhaa hizo iliyosafirishwa mwaka 2020 ni tani 170,000.”

Pia alisema kuna haja kwa serikali kuhamasisha uwekezaji kwenye miundombinu ya kusafirishia na kuhifahi mazao hayo kama vile nyama, maziwa na samaki ili kuyafanya mazao hayo yanayoharibika kwa haraka kufikishwa sokoni haraka kwa kutumia ndege hiyo.

Mtaalamu wa masuala ya biashara na uchumi, Nebart Mwapwele alisema ujio wa ndege hiyo utakuza biashara kwa kuwa itarahisisha usafirishaji wa bidhaa zinazoharibika haraka kuyafikia masoko ya nje.

Mwapwele alisema ili ndege hiyo itumike ipasavyo, kuna haja ya kufanyika uhamasishaji kwa Watanzania kujikita kwenye uzalishaji wa mazao yanayoharibika haraka kama maua, mbogamboga, samaki na nyama.

Pia alisema viwanda vya bidhaa hizo vilivyositisha uzalishaji vingeanza uzalishaji tena na wenye uwezo wawekeze kwenye ujenzi wa vyumba vya baridi vya kuhifadhia bidhaa hizo kwenye viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Kilimanjaro,  Mwanza, Dodoma na Songwe.

Habari Zifananazo

Back to top button