“NILIKUWA naenda kuchukua viazi shambani nikiwa njiani ghafla alitokea mwanaume mmoja akanichukua kwa nguvu akanipeleka nyumbani kwake na kuniingilia kimwili bila ridhaa yangu,” inasikika sauti ya msichana wa miaka (19) Kulwa Jibila.
Kulwa ni Mkazi wa Manoni ,Wilaya ya Kishapu ,mkoani Shinyanga anasimulia habari ya kusikitisha ambayo imekatisha ndoto zake za kielimu na kuharibu mwelekeo wa maisha yake.
Mwanzoni mwa mwezi Februari,2023, Kulwa alizungumza na mwandishi wa makala hii na kumueleza madhila aliyoyapitia wakati alipomaliza shule ya msingi mwaka 2020.
Katika simuliza ya sababu za ugumu wa maisha yake anaeleza kuwa baada ya kumaliza shule ya msingi alitamani kuendelea na masomo au na elimu yoyote ya kumuendeleza, lakini ndoto zake ziligonga mwamba kutokana na kuolewa kwa nguvu.
“Mwanaume huyo baada ya kunichukua kwa nguvu na kuniingilia wakaenda kutoa taarifa nyumbani kwetu kuwa tayari nimeshaolewa, hivyo wazazi wakaja kupanga namna ya kutoa mahari, hivyo sikuwa na sauti ya kujiteteta niliolewa nikiwa na umri mdogo japo sikupenda,”anaeleza Kulwa.
Kulwa ambaye sasa ana mtoto mmoja wa miezi sita ametelekezwa na mwanaume aliyemuoa tangu akiwa na ujauzito wa miezi mitatu na anaishi na wazazi wake, ambao wamechukua nafasi ya kumlea pamoja na mtoto wake.
“Ilikuwa changamoto akienda huko ana wanawake wengi na sitamani tena kuolewa niliona nitapata magonjwa nikaondoka, pia alikuwa hanitunzi hata sabuni sipati alikuwa hana kazi,” anasema.
Kulwa anasema hatamani mtoto wake aliyenaye ambaye ni wakike apitie mazingira aliyopitia yeye na atamuandalia malezi mazuri ya kusoma na kujisimamia mwenyewe.
“Sasa najishughulisha na kilimo naishi na baba na mama na mwanaume hayupo ameondoka kabisa, nahitaji kufanya kazi na wasichana wanaotoka katika ndoa za utotoni wasaidiwe pia, ili waweze kuendesha maisha yao,”anasisitiza Kulwa.
WAZAZI WASIMULIA MACHUNGU YAO
Baba Mzazi wa Kulwa, Mzee Kiliga anasema mtoto wake aliolewa na mwanaume ambaye ametoroka kwenda Morogoro kwa mwaka mmoja sasa.
Anasema kuhusu binti yake kupotea hawakwenda polisi na walikuwa wanamtafuta kijijini taarifa zikafika kwake kuwa ameshaolewa.
“Kwanza alimwacha akiwa mjamzito hadi kajifungua hayupo, karudi nyumbani nikamtunza hadi sasa niko nayo,ametelekezwa natamani siku zirudi nyuma nirekebishe hili nisingepokea mahari kwani huyu mwanaume alikuwa hamtaki,”anajuta Kiliga.
Anasema binti yake alitolewa mahari nusu ambayo ni ng’ombe watatu huku walikubaliana ng’ombe 16 na walimuambia watatoa tena.
“Alimwambia binti yangu aje nyumba atamfata badala yake alikuja tu kumuona akaondoka, siku anakaribia kujifungua nikampigia simu akakubali lakini hajaja hospitali akatoroka akaenda Morogoro, kwa hiyo hata mtoto hamjui hadi leo,”anaeleza kwa huzuni.
Anaongeza: “Walipomchukua nilitamani kumfata kwani matokeo ya darasa la saba yalikuwa yametoka hivyo nilitamani aendelee baada ya kumfatilia ndugu wakanishauri kuwa nikubali kuchukua mahari, kwani tayari ana ujauzito.”
Mama mzazi wa Kulwa anasema sasa wanalea wao mtoto na mjukuu huku hali ya maisha ikiwa ngumu.
“Sasa mtoto anaishi maisha magumu na mimi sijashiriki alikuwa hataki kuolewa ila alilazimishwa,” anasema.
Anasema Kulwa ana wadogo zake watatu wa kike hatamani yaliyomkuta dada yao yawakute na wao, hivyo atajitahidi kuwalinda na kuwasomesha kwa bidii.
SHERIA YA NDOA YATAJWA KUCHANGIA
Kwa mujibu wa ripoti ya Jeshi la Polisi Tanzania ya Kipindi cha Januari hadi Desemba 2020 matukio ya mimba kwa wanafunzi yalikuwa ni 3,631 na kumzorotesha mwanafunzi masomo 970.
Katika Mkoa wa Shinyanga jumla wa watoto 656 walifanyiwa vitendo vya kikatili kati yao 212 walipata mimba wakiwa wanafunzi na 23 walizoroteshwa masomo.
Wakati Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inamtafsiri kuwa ni mtu yoyote mwenye miaka chini ya 18, Sheria ya Ndoa inaruhusu mtoto wa kike chini ya umri huo kuolewa
Mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Rebeca Gyumi ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa vinavyoruhusu mtoto kuolewa kwa idhini ya wazazi ,akiwa na miaka 15 na mahakama akiwa na miaka 14 ni vya kibaguzi na ni kinyume na Katiba.
Katika uamuzi huo, Mahakama Kuu iliamua kuwa Sheria ya Ndoa ipitiwe upya ili kuondoa ubaguzi na kukosekana kwa usawa kati ya umri wa chini wa ndoa kwa wavulana na wasichana.
Mahakama ilisema kuwa Kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kinakwenda kinyume na Ibara ya 12, 13 na 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inatoa haki sawa kwa wote mbele ya sheria.
Askofu Ambele Mwaipopo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Rukwa, anasema mkanganyiko wa sheria unatoa tafsiri nyingine kwamba mtoto wa kike ni mtu mwenye umri chini ya miaka 14 na wala sio miaka 18 tena.
Anasema kama sheria inamtaja mtoto kama ni mtu mwenye miaka chini ya 18 na inataja haki zake mbalimbali ikiwemo kuendelezwa kielimu, basi Sheria ya Ndoa inatoa mwanya au ni kichocheo cha ndoa na mimba za utotoni kwa kuwa inaruhusu mtoto kuolewa akiwa na miaka 14 au 15.
Ili kuondoa mkanganyiko huo, Askofu Mwaipopo anasema serikali haina budi kufanya marekebisho ya haraka ya sheria hiyo, ili kuwanusuru watoto wa kike wasipoteza haki zao ikiwemo Haki ya Kuendelezwa ambayo kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania; maendeleo hayo yanahusiana na mtoto kuwa na kiwango kinachokidhi makuzi kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii.
Anasema sheria ya Kanisa inatambua mazingira ambayo yanaweka vizuizi kwa watu wakiwemo watoto kufunga ndoa, hata hivyo sheria za nchi kwa upande mwingine zinawaweka njiapanda pale ridhaa ya wazazi au amri ya mahakama inapotolewa.
JE MILA NA DESTURI ZINACHANGIA NDOA ZA UTOTONI ?
Mila na desturi zinatajwa kuwa mojawapo ya sababu za ndoa za utotoni katika Mkoa wa Shinyanga, ambapo kitendo cha msichana Kulwa kuchukuliwa barabarani bila ridhaa yake inahusishwa na mila jamii hiyo.
Mzee wa mila Kasimu Kishiwa kutoka Kijiji cha Negezi, anasema kuchukuliwa mtoto wa kike bila ridhaa ya wazazi wake sio jambo sahihi, hivyo ameitaka jamii kubadilika
“Sisi kama wazee watu kama hao wanatengwa na jamii kwa sasa inakuwa kama sio ubinadamu wanatengwa katika jamii na vikao vya wazee anatengwa.
“Vijana mara nyingi ndio anafanya vitu kama hivyo na wazazi wengi huwa wanawanyang’anya ukikuta kwao wana mali wanamwacha.”
Anasema Sasa kuna vikao ,warsha mbalimbali vya kimila na serikali na matukio kama hayo yamepungua hivyo kadiri watu wanavyopata elimu mabadiliko yanaonekana.
Mzee wa mila mwingine ,Mikael Ngelela anasema ndoa za utotoni zinatokana na namna jamii inavyoishi katika mifumo yao.
“Katika hili pia wazazi kuwa na tamaa ya kupata mahari inatajwa kwani kuna wazazi huwaozesha mabinti zao katika umri mdogo wakiamini kupata mahari.
” Wakati umefika wakuachana na mila potofu huwa kuna mikutano tunakaa wanaelimisha hata kama ni mashuleni picha halisi wazazi na watoto wanayo ,”anaeleza Mzee Ngelela.
DINI HAZIUNGI MKONO NDOA ZA UTOTONI
Shekhe Othuman Ndamo anasema wazazi wapewe elimu kuhusu namna bora ya kulea watoto na kulelewa
“Sisi kidini kama mtoto wa kike ukimjenga unajenga jamii mzima na ukimharibu umeharibu jamii wana nafasi ya kujengewa mwanzo bora wa kulea familia , dini inachukua jukumu la kumuelisha haki ya mtoto kwa mzazi hasa kupewa chakula , malazi na mambo mengi.”
Anasema wanaielimisha jamii imrudiee Mungu na wazazi kutekeleza wajibu wao na elimu kupewa kipaumbele.
Kwa upande wake Mchungaji Yohana Dada wa Kanisa la AIC, anaeleza kuwa wanaendelea kuelimisha jamii kwani ndoa za utotoni zinaleta matatizo mengine.
“Watu wamwombe Mungu kuwa waondolee na tamaa kwa watoto na wazazi wawalee watoto wao katika kumjua Mungu na kuwa na hofu na inayompendeza Mungu, ili kuacha mambo yasiyofaa na mtoto akifikisha miaka 18 apate mchumba na aolewe kwa kufunga ndoa kanisani hii ndio inampendeza Mungu,”anasisitiza.
MADHARA YA NDOA ZA UTOTONI
Rose Mlay ni Mratibu Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe wa uzazi salama, anasema ndoa za utotoni zina madhara kwa sababu mtoto chini ya miaka 18 hajaweza kufanya maamuzi na bado anaendelea kukua na viungo vyao havijakomaa.
“ Kwa hiyo akiolewa unakuta anapata ujauzito, kwanza akili haijakomaa hata kwenda kliniki shida, lakini wakati wana mimba wengi wanaopata kifafa cha mimba ni wale wadogo anaweza akafa.
“Lakini wanapokwenda kujifungua mtoto anaweza asitoke kwa sababu nyonga bado ni ndogo matokeo yake anaweza kujilazimisha akapata fistula mkojo unatoka wenyewe na kinyesi, lakini pia mtoto anaweza akazaliwa amekufa au utindio wa ubongo na mama anaweza kupoteza maisha,”anaeleza.