Ndondole mbaroni kwa kukutwa na meno ya tembo

NJOMBE: JESHI la Polisi Mkoa wa Njombe, linamshikilia Vinord Ndondole ,37, mkazi wa Matemela Mbalali Mbeya kwa tuhuma za kukutwa na meno manne ya tembo yenye thamani ya Sh 197,280,000 akiwa anayasafirisha kwa pikipiki.

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 13, 2025 na Jeshi la Polisi, ambapo limesema Ndondole amekamatwa katika operesheni zake na misako inayoendelea mkoani humo yenye lengo la kuimarisha usalama.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linanshikilia Vinord Lucas Ndondole kwa kosa la kupatikana na nyara za serikali meno ya Tembo manne akiwa ameyafunga ndani ya mfuko wa salfet kwenye pikipiki yake akiwa anasafirisha kama mzigo wa kawaida. Meno yana thamani ya Tsh 197,280,000” Imeeleza taarifa hiyo.

Wakati huohuo katika operesheni hiyo Jeshi hilo pia limewakamatwa watuhumiwa wengine 55 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya wizi wa pikipiki, uporaji, uvunjaji, wizi wa kawaida, wizi wa mitandao na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

“Katika operesheni na Misako iliyofanyika katika kipindi cha mwezi Januari 2025, Watuhumiwa wengine 55 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya wizi wa pikipiki, uporaji, uvunjaji, wizi wa kawaida, wizi wa mitandao na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani” Imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imetaja vielelezo mbalimbali vilivyokamatwa katika opersheni hiyo ni pamoja na kompyuta, CPU, kamera, stendi za kamera, mwamvuli mkubwa, kisimbuzi cha azam, ipad na viatu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button