Neema yazidi kunukia uwekezaji Pwani

TANZANIA inatarajia kuingiza Dola za Marekani Milioni 148 ambazo ni karibu Sh bilioni 352.2,  mara baada ya kukamilika ujenzi wa viwanda viwili vya kigeni kutoka China.

Viwanda hivyo ni Saphier Glass na Keda Glass Factory, ambapo kila kiwanda asilimia 25 ya uzalishaji wake utakuwa kwa ajili ya soko la ndani huku asilimia 75 zitauzwa soko la nje.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Uwekezaji Dk. Tausi Kida, katika ziara yake kutembelea miradi ya kimkakati Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, ambapo amesema zaidi ya asilimia 80 ya malighafi zitakazotumika zitatoka nchini.

Advertisement

Pia amesema ajira 7,000 zitazalishwa kutoka katika kila kiwanda pale ujenzi utakapokamilika, ambapo hadi sasa zaidi ya watu 850 wameshaajiriwa kupitia ujenzi unaoendelea kupitia viwanda hivyo.

“Tumefarijika uwekezaji huu mkubwa unakwenda vizuri na changamoto zote zilizokuwepo za maji na umeme zimeshatatuliwa ikiwemo zile za ukinzani wa sheria ya fedha na uwekezaji zimepatiwa majibu kupitia sheria mpya ya uwekezaji iliyopitishwa Desemba mwaka jana, hivyo Tanzania na nchi wanachama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC wanakwenda kufaidika na miradi hii,” amesema.

Dk. Kida ameongeza kuwa kiwanda cha Saphier kimewekeza zaidi ya dola za Marekani milioni 310, ambayo ni sawa na Sh bilioni 740 na kinatarajia kuanza kazi Septemba mwaka huu, wakati kile cha Keda uwekezaji wake ni dola za Marekani milioni 300, ambazo ni sawa na Sh bilioni 713, huku kikitarajiwa kukamilika na kuanza uzalishaji Januari 2024.

Naye mwenyeji wa ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Khadija Nassir, amesema wilaya yake ni miongoni mwa wilaya zenye viwanda vingi lakini hilo halitoshi kuleta tija itakayopatikana kupitia viwanda hivyo, bila mikakati thabiti katika kuandaa mazingira rafiki ili kushawishi wawekezaji wengi.

“Leo tupo hapa katika kiwanda cha Saphier kiwanda ambacho ni cha kwanza Tanzania na Afrika Mashariki na hii ni katika matokeo ya juhudi na dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia kuhakikisha sekta ya uwekezaji inakua nchini,”  amesema.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *