DAR ES SALAAM: BARAZA la Usimamizi wa Mazingira la Taifa (NEMC) limeanzisha jukwaa la kuwakutanisha na kuwashirikisha wadau wa masuala ya bahari kujadili usimamizi endelevu wa bahari ili kuwa na mifumo ya sera na fursa za uchumi wa buluu.
Akizungumza katika mkutano wa Kwanza wa Usimamizi wa Bahari wa Tanzania uliofanyika leo Februari 18, 2025 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi wa Zanzibar, Zahor Elkharousy amesema lengo ni kuwaleta pamoja wadau, kujadili changamoto na kuchangia mawazo kwa manufaa ya bahari.
“Mkutano huu tumeuita kwa ajili ya kushirikisha wadau tofauti wanaoshughulika na masuala ya bahari ili wazungumze changamoto na kusaidiana mawazo jinsi ya kuhakikisha tunapata manufaa kutokana na bahari lakini wakati huohuo tunahifadhi bahari yetu kama inavyotakiwa,” amesema Elkharousy.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu – Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Christina Mndeme amesema mkutano huo ni muhimu kwa serikali kwa sababu bahari inachangia ukuaji wa uchumi wa nchi, hivyo mkutano huo utawawezesha wadau hao kubadilishana uzoefu wa namna ya kutumia bahari.
Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa NEMC kwa kuanzisha jukwaa hilo kwa kuwa itasaidia kusimamia sekta ya bahari kwa kiwango kikubwa na kuinua fursa zinazopatikana katika bahari.
“Mkutano huu unaumuhimu sana kwa serikali sote tunafahamu Bahari na Pwani yake ni kiungo muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa nchi, katika mkutano huu tunakwenda kubadilishana mawazo na kupata uzoefu kutoka kwa wadau mbalimbali.
Tunakwenda kuanzisha jukwaa hili muhimu tukiamini kwamba tunakwenda kuiangalia bahari kama kitovu cha Uchumi. Pia itasaidia kusimamia sekta ya bahari kwa kiwango kikubwa na kuinua fursa mbalimbali zinazopatikana katika bahari yetu,” amesema Mndeme.
Dk. Immaculate Semesi, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, amesema Jukwaa hilo la usimamizi wa rasilimali ya bahari na pwani litajumuisha sekta mbalimbali za serikali na zisizo za serikali pamoja na wadau wa maendeleo ili kuwezesha Uchumi wa Buluu ulioendelevu na wenye manufaa nchini.