NEMC yatafiti kuoza mifuko mbadala

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema linaendelea kutafi ti uwezo wa kuoza mifuko mbadala.
Mkurugenzi Mkuu NEMC, Dk Immaculate Sware Semesi amesema hayo Dodona wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Dk Semesi alisema utafiti huo unafanyika kuainisha ubora na viwango vinavyotakiwa kuzingatiwa katika utengenezaji wa mifuko mbadala isiyo ya plastiki ili kujua uwezekano wa mifuko hiyo kuwa na uwezo wa kuoza.
Pia, alisema NEMC imefanya tathmini na kuandaa ripoti zenye ushauri wa namna ya kutatua changamoto mazingira kwenye maeneo mbalimbali kama vile mafuriko kwenye maeneo ya Rufiji na Singida na Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Dk Semesi alisema pia NEMC imefanya tathmini na kuandaa ripoti zenye ushauri wa namna ya kukabili maporomoko ya udongo kwenye maeneo ya milima ya miamba Myamba (Same), Mlima Kawetere na Mlima Livingstsone (Mbeya), na Mlima Hanang (Manyara); Changamoto za mazingira kwenye bandari bubu; na tathmini ya hali ya mazingira kwenye maeneo oevu kama vile Kilombero na Malagarasi Moyovosi.
Pia, alisema kwa kipindi cha miaka minne, NEMC imefanya tafiti na kuandaa maandiko ya miradi.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa NEMC imeratibu utekelezaji wa miradi ya mabadiliko ya tabianchi, kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu na mradi wa kusimamia utekelezaji wa sheria ya mazingira.
Dk Semesi alisema ajenda ya tafiti imetekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja utafiti kuhusu changamoto za uchafuzi wa Mto Mara, mmomonyoko wa fukwe za maeneo ya fukwe ya Coco, fukwe ya Kunduchi, fukwe ya Klabu ya Mbweni JKT, Kikosi cha Jeshi Wanamaji 742, fukwe za Mikadi, eneo la Msuka lililopo Pemba Kaskazini, Ghuba ya Mikindani na Manispaa ya Mtwara.
“Vilevile Baraza limefanya tathmini ya hali ya mazingira kwenye maeneo yanayokumbwa na maporomoko ya ardhi katika milima ya Hanang, Manyara na Mamba Myamba iliyopo Wilayani Same–Kilimanjaro,” alisema Dk Semesi.
Alisema NEMC imefanya tathmini ya ubora wa maji ya Ziwa Victoria na kuaianisha maeneo yanayotakiwa kupewa kipaumbele katika suala la kulinda ubora wa maji kutokana na athari zilizobainika katika ziwa hilo.
Dk Semesi alisema katika utekelezaji wa miradi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi kupitia ithibati ya kuwa msimamizi wa fedha za Mfuko wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabianchi nchini, NEMC imeratibu maandiko na utekelezaji wa miradi minne.
Aliitaja miradi hiyo ni pamoja na wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi wilayani Bunda mkoani Mara na mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii za wakulima na wafugaji wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma.
Mingine ni mradi wa kuainisha na kutumia teknolojia za kimkakati za uvunaji maji ili kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika maeneo kame ya Tanzania (mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora) na mradi wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii za pwani Zanzibar.