NFRA: Nchi ina chakula cha kutosha

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umesema una akiba ya kutosha ya chakula katika maghala yake.
Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dk Andrew Komba amesema wameongeza uwezo wa kuhifadhi chakula cha akiba na kuuza takribani tani 600,000 za mazao katika masoko ya kimataifa.
Dk Komba aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam hivi karibuni kuwa katika kipindi cha Julai hadi Novemba mwaka jana, NFRA ilinunua tani 479,000 kwa wakulima na kiasi hicho hakikuwahi kufikiwa katika taasisi hiyo katika miaka ya nyuma.
Alisema NFRA ina jumla ya tani 776,000 katika maghala yake na kati ya hizo, tani 400,000 zitauzwa katika masoko ya ndani na nje na tani 300,000 zitahifadhiwa katika maghala kwa ajili ya kulinda usalama wa chakula nchini.
Dk Komba alisema endapo uzalishaji wa chakula kutoka kwa wakulima utapungua, NFRA itakuwa na uwezo wa kuilisha nchi kwa mwaka mzima.
“Kwa sasa NFRA ina shehena ya kutosha ambayo itaiwezesha nchi kufanya biashara ya kuuza mazao katika masoko ya ndani na nje, pia itaendelea kuwa na shehena ambayo itasaidia kulisha nchi endapo majanga ya njaa au maafa yatatokea,” alisema.
Alisema katika miaka ya nyuma, NFRA ilikuwa na uwezo wa kuuza kati ya tani 50,000 na 60,000 katika masoko ya kimataifa lakini uhifadhi wa akiba ya chakula umeongezeka.
“Lakini pia tumeweza kuuza nje ya nchi chakula cha ziada na hii imesaidia kuinua maisha ya wakulima wetu na nchi kupata faida kutokana na mauzo hayo ya nafaka ya nje ya nchi,” alisema Dk Komba.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024, NFRA ilikuwa na uwezo wa kuhifadhi shehena ya tani 351,000 lakini hadi kufikia sasa uwezo wa taasisi hiyo umeongezeka hadi kufikia kuhifadhi tani 776,000.
Dk Komba alisema NFRA imekusanya takribani Sh bilioni 540 ya mauzo ya nafaka na fedha hizo zimekuwa zikitumika kupanua maeneo ya utendaji ukiwemo ukarabati wa miundombinu na maghala.
“Mafanikio haya yanatokana na mizunguko ambayo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akiifanya katika nchi tofauti, akitumia nafasi hiyo kuinadi NFRA na kusaidia kupata masoko ya uhakika kwa nchi zenye uhitaji wa chakula,” alisema.
Dk Komba alisema kupitia Wizara ya Kilimo, serikali imeiwezesha NFRA kuwa na maghala yenye uwezo wa kutunza jumla ya tani 48,000.
“Rais Samia akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma mwaka jana, alitukabidhi jumla ya maghala 28 yenye uwezo wa kuhifadhi takribani tani 28,000 hivyo serikali kupitia wizara imetusaidia ujenzi wa maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani takribani 76,000 za chakula,” alisema.
Dk Komba alisema NFRA katika mwaka wa fedha uliopita, ilizindua maghala mengine mawili yaliyojengwa katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
“Ili kuhakikisha nchi inakuwa na hifadhi ya chakula cha kutosha, Rais Dk Samia aliiwekea NFRA malengo ya kuwa na uwezo wa kuhifadhi tani milioni tatu ifikapo mwaka 2030,” alisema.



