NHIF yatoa ufafanuzi mabadiliko usajili kwa watoto

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unafanya maboresho ya utaratibu wa usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya ya Toto Afya Kadi kwa lengo la kuwafi kia watoto wengi ambao wako nje ya huduma.

Kutokana na maboresho hayo wazazi au walezi wanashauriwa kuwasajili watoto wao kama wategemezi wao kwenye Bima ya Afya au kusajili kupitia shule wanazosoma.

Advertisement

Mtendaji Mkuu wa NHIF, Bernard Konga alisema hayo Dodoma jana wakati wa kufafanua utekelezaji  wa mpango huo ambao umeanza Machi 13, mwaka huu.

Konga alisema hatua hiyo ni kuongeza wigo wa wanachama katika mfumo wa bima ya afya kuelekea bima ya afya kwa wote na kuhakikisha wanachama katika makundi hayo wanajiunga kama familia au kaya au makundi ya wanafunzi kupitia shule wanazosoma.

“Mpango wa Toto Afya Kadi ulianza mwaka 2016 ikiwa na lengo la kuwafikia kundi kubwa la watoto walio chini ya miaka 18 ambao kitakwimu ni zaidi ya nusu ya wananchi wote ili kufikia azma ya serikali ya watu wote kuwa na bima ya afya,” alisema.

Konga alisema tangu kuanza kulihudumia kundi la watoto kwa kipindi cha miaka saba sasa, mfuko umefikia watoto 210,664 walio chini ya miaka 18.

Alisema NHIF imekuwa ikishirikiana na shule za msingi na sekondari ili kusajili wanafunzi na mwitikio unaonesha ni njia sahihi ya kuendelea nayo ili watoto wengi zaidi wasajiliwe na kunufaika na bima ya afya.

Konga alisema pia kundi la watoto watakaokosa sifa na vigezo vya kuandikishwa kupitia bima za wazazi kwa mwajiri au vifurushi wanaweza kuandikishwa kupitia vyuo, shule au vituo rasmi vya kuelekea watoto waishio katika mazingira magumu.