Ni suala la muda tu Kampasi ya UDSM Kagera

DAR ES SALAAM: CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kimetiliana saini na Kampuni ya China Jiangxi Corporation for International Econamic and Technical Cooperation, ya mkataba wa kujenga majengo manne katika Kampasi ya Kagera.

Ujenzi huo ni kupitia Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi katika Elimu ya Juu (HEET).

Akizungumza kabla ya utiaji saini huo, Mgeni Rasmi katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amesema kwa kujenga majengo hayo, uwepo wa wanafunzi katika mkoa huo, utachachua biashara na kuufanya uchumi kukua.

“Kwa ujenzi wa chuo hiki, wageni kutoka nchi jirani watakuja, elimu tutanufaika nayo, lakini ajira zitaongezeka. Kagera tumejipanga kwa kuwa mradi huu tunaupenda,” amesema.

Isome pia: https://habarileo.co.tz/heet-kuboresha-miundombinu-udsm/

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo amesema, kuanza kwa shughuli za ujenzi ni hatua kubwa na mafanikio ya kujivunia katika kufanikisha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa elimu ya juu nchini na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Hongereni sana! Ni matumaini yangu kwamba Kampuni ya Mhandisi imekamilisha kazi ya mapitio ya michoro na sasa wapo tayari kuanza usimamizi mara baada ya mkataba wa ujenzi kusainiwa,” amesema.

Amesema serikali itaendelea kuratibu, kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa mradi huo.

“Tutaendelea kuwahimiza kuongeza kasi ya utekelezaji. Pale mtakapoona mnakwama kwa sababu yoyote ile muwe wepesi kuwasiliana nasi ili tuona namna nzuri ya kukwamua mchakato,” amesema.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amesema majengo hayo yatakayojengwa ni sehemu ya majengo 25 yanayojengwa kupitia mradi huo wa HEET.

Amesema  kuanzishwa kwa Kampasi ya Kagera ni matokeo ya juhudi za serikali za kuhakikisha Watanzania wengi wanafikiwa na elimu ya juu.

Habari Zifananazo

Back to top button