SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) halikutumia njia ya ununuzi ya ushindani katika ujenzi wa reli ya kisasa kwa kipande cha tatu na cha nne na kusababisha kuongezeka kwa Dola za Marekani milioni 1.3 na milioni 1.6 kwa kilomita ikilinganishwa na mikataba ya awali.
Kuongezeka kwa gharama ya ununuzi wa treni na mabehewa ya abiria kwa jumla ya Dola za Marekani milioni 215.05 (Sh. bilioni 492.46), na Euro milioni 4.53 (Sh. bilioni 11.59) kutokana na usimamizi duni wa mikataba.
Vile vile mkataba ulitekelezwa bila kuwepo kwa dhamana ya utendaji, hali iliyosababisha hasara ya kiasi cha Euro milioni 5.32 (Sh. bilioni 13.6), na kutotoza gharama za uchelewashaji wa kazi kwa mujibu wa mkataba.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere imebaini kuwa na viashiria vya kutumia Dola za Marekani milioni 11.19 (Sh. bilioni 25.62) zaidi ya kiwango kilichopangwa kutoka fungu la fedha za dharura katika ujenzi wa reli ya kisasa kipande cha kwanza kutokana na kuongezeka kwa muda wa ujenzi wa reli kwa zaidi ya siku 1441, hiyo imesababisha kuongezeka kwa gharama ya Mhandisi Mshauri wa mradi kwa Dola za Marekani milioni 11.32.
Aidha ripoti hiyo inasema kuwa CAG amebaini upungufu katika usimamizi wa vibali vya raia wa kigeni.
“Zaidi ya hayo, kutokuwepo kwa nyaraka za mikataba kwa baadhi ya miradi. Kushindwa kudai msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani Sh. bilioni 4.27 na madai ya riba ya Sh. bilioni 12.12 iliyotokana na kuchelewa kulipa wakandarasi,” imesema ripoti hiyo.
Pia, malipo zaidi ya Sh. milioni 562.68 na Sh. milioni 584.68 mtawalia yaliyotokana na makadirio ya gharama yasiyojitosheleza kwa nguzo za kusimikwa ardhini. Malipo ya awali Sh. milioni 857.21 na Sh. bilioni 4.83 hayakurejeshwa na yalilipwa bila kuwepo kwa matakwa ya kimkataba.
Aidha, ujenzi wa reli ya kisasa ilibainika ukosefu wa viwango maalum kwa kazi ya mfumo wa umeme kwa ajili ya makandarasi kufanya nukuu za bei na makadirio ya gharama za mradi wa umeme hayakuzingatia sanifu na tafiti za awali.
Zaidi ya hayo hakukuwa na muda uliopangwa wa kukamilisha ujenzi wa karakana ya kuunganisha treni za umeme za kisasa.