‘Nyerere alionesha njia kushughulikia wakimbizi Afrika’
MWALIMU Julius Nyerere, mbali na kuonesha njia kuhusu kushughulikia na kusimamia hifadhi ya wakimbizi, mawazo yake yalisaidia katika kuandika mkataba wa wakimbizi na wahamiaji wa mwaka 1969 wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).
Haya yalielezwa jana kwenye mjadala kuhusu ushiriki na mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika kushughulikia wahamiaji na wakimbizi ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya wakimbizi la Dignity Kwanza kama sehemu ya kuadhimisha miaka 23 ya kuishi bila Nyerere.
Akiwasilisha mada katika mjadala huo uliohusisha wahariri wa vyombo mbalimbali, Profesa Khoti Kamanga kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema kabla ya Mkataba huo wa OAU (sasa Umoja wa Afrika -AU), tafsiri ya nani mkimbizi na mhamiaji ilikuwa inatolewa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki ya Wakimbizi wa mwaka 1951.
Profesa Kamanga ambaye ni mwalimu wa sheria UDSM, alisema mkataba huo wa kimataifa ulikuwa hautoi tafsiri sahihi kuhusu wakimbizi na wahamiaji kulingana na mazingira ya Afrika kama vile wapigania uhuru au watu wanaokimbia nchi zao kutokana na kutawaliwa na viongozi dhalimu.
“Kwa tafsiri ya Mkataba wa Afrika wakimbizi na wahamiaji wengi waliohifadhiwa Tanzania wasingekuwa na hadhi hiyo. Kwanza Mkataba huo ulikuwa hautumbui watu wanaokimbia nchi yao kwa makundi na pia ulikuwa unatambua jeshi ni kati ya nchi moja na nyingine na siyo kati ya jeshi la nchi na kundi fulani ndani ya nchi moja,” alisema.
Alisema Mwalimu Nyerere alianzisha sera ya kufungua milango kwa wakimbizi na watafuta makazi (open door policy) ili kusaidia; wapigania uhuru wakati wa vita vya ukombozi wa Bara la Afrika, wakimbizi waliotokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na watu waliowakimbia watawala dhalimu.
Profesa Kamanga alisema kilichomsukuma Nyerere kuja na sera hiyo ni kutokana na tabia yake ya kuheshimu haki na kuamini kwamba ana jukumu la kupambana na kila aina ya dhuluma na ubaguzi.
“Mwalimu aliamini pia kwamba Afrika ni moja na hakukubali mipaka iliyowekwa na wakoloni na ndio maana akaja na sera hii ingawa haikuwa imeandikwa,” alisema.
Naye Mbunge wa zamani wa Kasulu, Daniel Nsanzugwanko alisema Mwalimu Nyerere ni mtu aliyepigania sana utu wa mwanadamu na alipaswa kupewa tuzo ya Nobeli lakini alipofuatilia akagundua kwamba alinyimwa tuzo hiyo kwa sababu tu ya kuwa mjamaa.
Mwanasiasa huyo ambaye alisema ameishi na wakimbizi kwa muda mrefu aliwataka Watanzania kutojenga dhana mbaya kila wanaposikia neno ‘mkimbizi’ likitajwa wakiamini ni mtu hatari.
Alisema wakimbizi wanapolazimika kukimbia nchi zao hawafanyi hivyo kwa kupenda na siyo watu wajinga bali ni watu ambao huja na maarifa yao, ujuzi wao na nguvu zao ambazo Watanzania tunapaswa kunufaika nazo.



