Nyota wa Yanga ajitosa ubunge Iringa Mjini

IRINGA: MWANASOKA wa zamani wa timu ya Yanga SC, Ally Msigwa, amejitosa rasmi katika mbio za kisiasa baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Msigwa, mzaliwa na mkazi wa Manispaa ya Iringa, amesema wakati wa kuchukua fomu hiyo kuwa yupo katika siasa si kwa matamanio binafsi bali kwa nia thabiti ya kubadilisha maisha ya watu wa Iringa, hasa vijana.
“Nimecheza mpira katika kiwango cha juu, nimekumbatia ndoto yangu na kuishi maisha ya kujituma. Sasa nimeamua kuwekeza uzoefu wangu katika siasa, ili kutoa dira mpya kwa vijana wa Iringa,” amesema Msigwa.
Ally Msigwa si jina geni kwa wapenzi wa soka. Akiwa beki wa kati wa kuaminika, aliwahi kuichezea klabu kongwe ya Yanga SC na kuwa sehemu ya mafanikio ya timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
SOMA ZAIDI
Lakini nyuma ya mafanikio hayo, Msigwa alijijengea taswira ya mchezaji mwenye maadili, anayejali jamii na mwenye ndoto kubwa nje ya dimba.
“Nikiwa mchezaji, niliona namna ambavyo vijana wanahitaji hamasa na dira. Katika siasa nitahakikisha vijana wa Iringa wanakuwa na majukwaa ya kuibua vipaji, kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii,” alieleza.
Akizungumzia chimbuko lake, Msigwa alisema: “Mimi ni mzaliwa wa Iringa Mjini. Hapa ndiko nilikokulia, nikasoma, na kuanza safari ya ndoto yangu kupitia mpira wa miguu. Najua kilio cha vijana, najua changamoto za mama lishe, najua juhudi za waalimu, wafanyabiashara na wazazi. Naelewa pia fursa tulizonazo.”
Msigwa anaamini kwamba taaluma ya michezo inaweza kuwa daraja muhimu kuelekea kwenye uongozi bora.
“Uwanjani, nilijifunza nidhamu, kujituma, na kufanya kazi kama timu. Hayo ndiyo mambo ambayo ninataka kuyapeleka bungeni,” alisema.

