Nyumba nyingine 5,000 kujengwa Msomera

TANGA; Handeni. Makatibu Wakuu wa wizara za kisekta wamefanya ziara katika Kijiji cha Msomera, Wilaya ya Handeni mkoani Tanga katika eneo la mradi linalotarajiwa kujengwa nyumba nyingine 5000, kwa ajili ya watu wanaohama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Akizungumza kwa niaba ya Makatibu Wakuu wenzake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbas, amesema serikali itaendelea na azma yake ya kuwawezesha wananchi hao kuhama kwa hiari, ambapo sasa nyumba 5000 zitajengwa kwa ajili yao.

Tayari serikali imeshatekeleza awamu ya kwanza ya ujenzi iliyohusisha nyumba 503, Kituo cha Polisi, nyumba ya malazi ya Askari polisi, ukarabati wa zahanati ya kijiji, shule ya msingi na sekondari.

Pia kuna miundombinu mingine ya maji, majosho, barabara, umeme na mawasiliano iliyojengwa na kukamilika.

Dk Abbas amesema serikali ina nia thabiti ya kuwawezesha wananchi hao kuondoka kwa hiari, ili kupisha maboresho ya shughuli za uhifadhi Ngorongoro.

β€œNia na dhamira ya serikali ni kuhakikisha inakamilisha zoezi la ndugu zetu wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro kuja hapa Msomera, tulianza awamu ya kwanza na sasa awamu ya pili ishatangazwa na sisi tumekuja kushuhudia maandalizi ambayo yapo tayari kwa ajili ya kazi hii …lengo letu ni kujenga nyumba 5000,” amesema Dk. Abbasi.

Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Kanali Petro Ngata, amesema ujenzi wa nyumba hizo utakamilika ndani ya miezi sita kama ilivyoelekezwa na serikali.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando ametoa pongezi kwa makatibu wakuu waliofika katika eneo hilo, huku akiahidi maelekezo yote yaliyotelewa na viongozi yatatekelezwa kwa wakati.
Ujenzi wa nyumba hizo unatarajiwa kuanza Oktober Mosi, 2023 na kukamilika ndani ya miezi sita.

Habari Zifananazo

Back to top button