Nyumba za kifahari zakamatwa Nigeria

NIGERIA : TUME ya Uhalifu wa Kiuchumi na Kifedha (EFCC) nchini Nigeria inazishikilia zaidi ya nyumba 750 katika mji mkuu, Abuja.

EFCC iliyoanzishwa mwaka 2003 ili kupambana na rushwa, haijafichua ni nani hasa mmiliki wa ardhi na nyumba hizo za kifahari, lakini taarifa  inasema ni za afisa wa zamani wa ngazi za juu serikalini.

Nyumba hizo zilizoko nje kidogo ya Abuja, ziko kwenye eneo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 150,000, na mtaalamu wa mali aliyeko Abuja anakadiria zinaweza kuwa na thamani ya mamilioni ya dola.

Advertisement

Ufisadi ni moja wapo ya tatizo kubwa nchini Nigeria licha ya uwepo wa sera za serikali zinazoahidi kukomesha tatizo hilo.

Nchi hiyo ni mojawapo ya nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi barani Afrika, lakini wakazi wake wachache tu kati ya wakazi milioni 225 ndio wamefaidika na utajiri huo.

Kwa sasa kuna kesi kadhaa za ufisadi mahakamani zinazohusisha maafisa wa serikali wa zamani na maafisa wa sasa. SOMA: IMF yaiomba Kenya kuchunguza ufisadi

Mei mwaka huu, aliyekuwa waziri wa usafiri wa anga, Hadi Sirika, alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa, pamoja na bintiye na mkwe wake.

Sirika alikuwa mmoja wa mawaziri wenye nguvu katika serikali ya Rais wa zamani Muhammadu Buhari.

EFCC inamshutumu kwa kutumia cheo chake kuinufaisha makampuni ya bintiye na mkwe wake na watatu hao walikana mashtaka na kuachiliwa  kwa  dhamana.