OCPD yajifunza mifumo ya kisasa uandishi wa sheria

WAANDISHI wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) wamefanya ziara ya mafunzo nchini Uingereza, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao katika Mkutano wa Jumuiya ya Waandishi wa Sheria wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Association of Legislative Counsel – CALC), Kanda ya Ulaya.
Ziara hiyo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa OCPD wa kuboresha utendaji wake kupitia mafunzo ya kimataifa, ubadilishanaji wa uzoefu, na ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika nyanja ya uandishi na urekebu wa sheria. Lengo kuu lilikuwa kujifunza mbinu, mifumo na teknolojia mpya za uandishi wa sheria ili kuongeza ufanisi na ubora wa kazi za ofisi hiyo nchini Tanzania.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu wa Sheria, Utafiti na Mafunzo wa OCPD, Rehema Katuga, amesema safari hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani imewapa fursa ya kuona kwa vitendo namna wenzao wa Uingereza wanavyotekeleza majukumu yao kwa kutumia mifumo ya kisasa na mipango madhubuti ya mafunzo.
“Tulipata nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Uingereza (Office of Parliamentary Counsel – OPC), ambapo tulijifunza jinsi wanavyofanya kazi kama taasisi huru lakini yenye uhusiano wa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hii imetupa mwanga juu ya namna tunavyoweza kuboresha mifumo yetu nchini,” amesema Katuga.
Ameongeza kuwa maafisa hao walijifunza pia namna nchi hiyo inavyoshughulikia masuala ya urekebu wa sheria na jinsi mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu za kisheria inavyorahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.
“Tunarejea nchini tukiwa na maono mapya. Tumepata somo la namna tunavyoweza kuimarisha matumizi ya teknolojia, kubuni mpango wa mafunzo endelevu kwa waandishi wa sheria, na kuhakikisha taratibu zote za uandishi wa sheria zinakuwa wazi, shirikishi na zenye ufanisi,” amesema Katuga.
Kwa upande wake, Alfred Nyaronga,Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika OCPD, amesema timu hiyo ilitembelea pia Ofisi ya Taifa ya Kumbukumbu ya Nyaraka (The National Archives) na kujifunza kuhusu mfumo wa kidigitali wa Lawmaker, unaotumika nchini Uingereza katika maandalizi, marekebisho na urekebu wa sheria.
“Mfumo wa Lawmaker ni wa kipekee kwa kuwa unawawezesha wadau wote wa uandishi wa sheria kuanzia wizara, bunge, ofisi ya mwandishi wa sheria hadi mpigachapa wa serikali kufanya kazi kwa pamoja katika jukwaa moja la kidigitali. Mswada unaweza kupitiwa, kurekebishwa na kupitishwa hatua kwa hatua hadi unapokuwa sheria kamili ndani ya mfumo huo,” amesema Nyaronga.
Amebainisha kuwa mfumo huo pia hutumika katika urekebu wa sheria (consolidation of laws) kwa kuruhusu sheria zilizofanyiwa marekebisho kuunganishwa moja kwa moja, jambo linalorahisisha upatikanaji wa matoleo mapya ya sheria kwa wananchi.
“Ni mfumo bora sana ambao umeleta mapinduzi makubwa katika uandishi wa sheria nchini Uingereza. Tumeshawishika kuona umuhimu wa kuanzisha mazungumzo ya ushirikiano nao, kwani wameonyesha utayari wa kujenga uwezo kwa watumishi wetu ili nasi tuweze kuanzisha mfumo wa kidigitali wa aina hiyo nchini,” ameongeza.
NayeKaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki Ubora kutoka OCPD,Bavoo Junus amesema pamoja na nchi za Magharibi kupiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia za kisasa, wameweza pia kushughulikia changamoto zinazotokana na mifumo hiyo kwa njia zinazoongeza ufanisi.
“Jambo muhimu tulilojifunza ni mfumo wao wa in-house training, ambapo waandishi wapya wa sheria hupata mafunzo ya ndani kutoka kwa waandishi wenye uzoefu. Hii imeongeza ubora wa kazi na kuimarisha ujuzi wa wataalamu wapya. Ni mfumo ambao OCPD tayari imeanza kuutekeleza na tunapanga kuufanya endelevu,” amesema Bavoo.
Ameongeza kuwa walijifunza pia kuhusu utaratibu wa kugawa majukumu katika timu maalum ndani ya ofisi ya OPC, ambapo kila timu inashughulikia sekta mahususi ili kuhakikisha kazi inaendelea bila kutegemea mtu mmoja. Mfumo huo, alisema, umeongeza uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Wataalamu hao kutoka Tanzania pia walitembelea Bunge la Uingereza, likijumuisha House of Commons na House of Lords, ambapo walijifunza kuhusu utendaji wa vyombo hivyo vya kutunga sheria, taratibu za vikao, na historia ya bunge hilo lenye urithi mkubwa wa demokrasia ya kisheria.
Uzoefu huo, kwa mujibu wa washiriki, umefungua ukurasa mpya katika juhudi za OCPD kuboresha mifumo yake ya ndani, hasa katika maeneo ya uandishi wa sheria, urekebu wa sheria, ufasili wa sheria, na usimamizi wa kumbukumbu kwa kutumia teknolojia za kisasa.