KIONGOZI wa Muungano wa Azimio la Umoja Kenya, Raila Odinga amesema hatishiki na vitisho kutoka kwa rais wa nchi hiyo na maofisa wengine wa serikali; na kusisitiza maandamano ya nchi nzima yatafanyika kama ilivyopangwa Jumatatu ijayo.
Akizungumza katika Uwanja wa Mazembe jijini Nakuru, Odinga alisema maandamano yatakuwa ya amani.
“Hatuwezi kutishwa na William Ruto na Rigathi Gachagua. Nataka kuwaambia kwamba nilipigania ukombozi wa pili katika nchi hii wawili hao hawawezi kuelewa nilichopitia nilikamatwa, nikashitakiwa mahakamani na kwenda jela mwaka 1983, lakini nikaachiwa kwa kukosa ushahidi. Nimekuwa nikipigania demokrasia na nimewekwa kizuizini kwa miaka minane wakati baadhi yao walikuwa bado wananyonya,” alisema Odinga.
“Simba (Moi) aliogopwa, lakini tuling’oa meno yake. Niko tayari na nimejitayarisha kulipa gharama kubwa huku nikipigania ukombozi wa Kenya,” aliongeza Odinga huku kukiwa na shangwe kutoka kwa umati uliojaa kumsikiliza.
Odinga alizitaja sababu kuu sita ambazo zimemsukuma kufanya maandamano ikiwamo kukataa kwa Rais Ruto kuruhusu ukaguzi wa seva za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Sababu zingine ni kupinga kupanda kwa gharama ya maisha baada ya serikali kuondoa ruzuku, upendeleo katika utawala wa Kenya, kukosa kushauriana na wadau wengine katika uundaji upya wa IEBC na ahadi zisizotekelezwa na serikali hiyo.
Comments are closed.