OleNgurumwa ataka lugha ya staha kuelekeka Uchaguzi Mkuu
DAR ES SALAAM: MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umehimiza uvumilivu wa kisiasa na matumizi ya lugha ya staha kuelekea uchaguzi mkuu, huku ukikemea matumizi ya nguvu katika kushughulikia masuala ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi, ni jambo la kawaida kwa baadhi ya kauli kutoka kwa wanasiasa wa vyama mbalimbali kutowapendeza watu wengine, hivyo uvumilivu wa hali ya juu unahitajika.
“Katika siasa kujieleza ni sehemu ya chakula chake, hivyo ni muhimu kwa watu kuelewa na kuvumiliana. Hii haimaanishi kuwa kauli zisizo za staha zikubalike, bali kuna haja ya tahadhari na busara katika kutoa matamko,” amesema Olengurumwa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi, watetezi wa haki za binadamu na wanasiasa kuwa makini na kauli wanazotoa ili kuepuka kuingia katika migogoro ya kisheria isiyo ya lazima.
SOMA ZAIDI: Mufti: Tuepuke fitna, uzushi Uchaguzi Mkuu
Katika hatua nyingine, THRDC imesema imehuzunishwa na namna ilivyotumika kumkamata Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni huko Mbinga, mkoani Ruvuma. Olengurumwa amesema mazingira hayo hayakuwa mazuri na yangeweza kusababisha taharuki kwa waliokuwepo katika mkutano huo.
“Historia inaonyesha kuwa kuna matukio kama haya yaliyowahi kusababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na vifo, pale wanasiasa walipokamatwa kwa kutumia nguvu nyingi. Ni muhimu kuhakikisha kuwa sheria zinafuatwa bila kuvunja haki za msingi za binadamu,” amesema.
THRDC imevitaka vyombo vya dola kuacha kutumia nguvu za ziada na badala yake kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria. Mtandao huo umeonya kuwa matumizi ya nguvu dhidi ya wanasiasa au mikutano ya hadhara yanaweza kuwatia hofu wananchi na kuwafanya waogope kushiriki katika shughuli za kisiasa, hali itakayodhoofisha mchakato wa kidemokrasia nchini.



