Ongezeko la tembo mafanikio hifadhi ya Ruaha

MWAKA 2018 hadi 2021 umeelezwa kuadhimishwa kwa mafanikio makubwa katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, baada ya ongezeko la tembo 100 kuripotiwa, na kufanya idadi yao kufikia 15,608.

Akizungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya miaka 60 ya hifadhi hiyo, yaliyofanyika leo mjini Iringa kama sehemu ya sherehe za wiki ya maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Hassan Sulumbu, amesema:

“Hili ni ongezeko la kihistoria linaloashiria mafanikio makubwa ya juhudi za kupambana na ujangili na kulinda wanyamapori wetu. Tembo ni mali ya taifa na urithi wa vizazi vijavyo, hivyo ni jukumu letu kuwalinda na kuhakikisha wanaongezeka zaidi.”

Sulumbu aliongeza: “Tembo ni sehemu ya urithi wetu wa kipekee. Mafanikio ya leo ni ushahidi kuwa kwa juhudi za pamoja, tunaweza kulinda urithi huu wa thamani na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa sehemu salama la wanyamapori.”

Mkuu wa wilaya huyo alisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya serikali, wadau wa ndani na wa kimataifa, pamoja na jamii zinazozunguka Hifadhi ya Ruaha.

SOMA: Mambo makubwa yaja miaka 60 Hifadhi ya Ruaha

Ongezeko hili la tembo ni dalili ya juhudi za pamoja katika kuhakikisha maliasili za taifa zinahifadhiwa na kulindwa kwa manufaa ya kiuchumi na kiikolojia, amesema.

“Tembo hawa ni lulu ya utalii wetu. Ongezeko lao linaongeza thamani ya hifadhi ya Ruaha kama kivutio cha kimataifa, na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi yetu.”

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Godwell Ole Meing’ataki, amesema hifadhi hiyo, ambayo ni mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi barani Afrika, inategemea uwiano wa kiasili ili kudumisha bioanuwai yake.

Ameongeza kuwa tembo ni moja ya vivutio vikubwa kwa watalii katika hifadhi hiyo, kinachovutia watalii wa ndani na kutoka mataifa mbalimbali, hivyo kuchangia moja kwa moja pato la taifa kupitia utalii.

Meing’ataki amesema mafanikio haya ya ongezeko la tembo hayajaja bila changamoto na akafafanua kuwa katika miaka ya nyuma, tembo walikuwa wakipungua kwa kasi kutokana na ujangili wa pembe za ndovu.

Amesema takwimu zinaonesha mwaka 1977 hifadhi hiyo ilikuwa na tembo zaidi ya 40,000, lakini idadi hiyo ilipungua hadi 18,864 mwaka 1993, na kufikia 15,521 mwaka 2018.

SOMA: Ujenzi wa barabara ya Iringa, Hifadhi ya Ruaha waiva

Amesema serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi, iliweka mikakati thabiti ya kudhibiti ujangili, ikiwemo kuongeza doria, kutumia teknolojia ya kisasa kama ndege zisizo na rubani (drones), na kuimarisha ushirikiano na jamii zinazozunguka hifadhi.

“Hatua hizi zimeleta matokeo chanya. Ujangili umepungua kwa kiasi kikubwa, na sasa tunaona ongezeko hili la tembo ambao walikuwa kwenye hatari kubwa ya kutoweka,” ameeleza Meing’ataki.

Akiwasilisha mada kuhusu ongezeko la wanyamapori katika hifadhi hiyo, mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dk Hamza Kija, alisema sensa mpya waliyoikamilisha hivi karibuni inaonesha ongezeko zaidi la tembo na wanyama wengine ndani ya hifadhi.

Mada zingine zilizotolewa katika kongamano hilo ni pamoja na mipango ya utalii endelevu na rafiki wa mazingira, usimamizi wa maji na Mto Ruaha Mkuu, nafasi ya jamii katika uhifadhi, uvumbuzi wa teknolojia kwenye usimamizi wa wanyamapori na magonjwa ya wanyamapori.

Habari Zifananazo

Back to top button