KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa Ujenzi wa Uiwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ujenzi, Makamu Mwenyekiti wa PAC Japhet Hasunga amesema hayo baada ya kamati kutembelea na kukagua mradi huo pamoja na wajumbe wa kamati hiyo.

Hasunga ameitaka TANROADS kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa miundombinu ya uwanja huo ili ukamilike kwa wakati na ubora uliokusudiwa.
“Tumefurahi na tumeona maendeleo mazuri ya ujenzi wa kiwanja hiki kikubwa, tunampongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huu mkubwa ambao ameufanya.

“Ili tuweze kupima thamani ya fedha lazima tujue ni lini uwanja huu utakamilika na ukamilike kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa na kuanza kutumika, tunatamani kufikia mwezi wa saba uwe umekamilika,” amesisitiza Hasunga.
Aidha Hasunga ameongeza kuwa, “Eneo la kiwanja hiki ni kubwa lenye zaidi ya hekali elfu 11 hivyo litengwe eneo litakalotumika kwa ajili ya ujenzi wa hoteli, kumbi za mikutano na maduka makubwa (shopping malls) ili kuendelea kukuza utalii na kuchangamsha Uchumi wa Mkoa wa Dodoma”.

Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati hiyo Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa mradi huo umefikia asilimia 84 mpaka sasa na Mkandarasi anayetekeleza mradi huo atasimamiwa kikamilifu ili ukamilike kwa wakati.