DAR ES SALAAM: PACHA waliozaliwa wameungana na kutenganishwa katika Hospital ya Taifa ya Muhimbili wameruhusiwa kutoka hospitalini hapo.
Pacha hao waliozaliwa kwa nje wakiwa wameungana tumbo na kifua, ndani waliungana ini na mfupa wa kidari.
Akizungumza leo Februari 27, 2024 Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi, amesema uwekezaji wa kusomesha watalaam, kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa vya uchunguzi vya kisasa umeiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma zinazolingana na hadhi yake.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH, Dk Victor Ngota ameeleza kuwa upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao, ulichukua saa sita na kuhusisha jopo la madaktari wazawa wenye utaalam mchanganyiko ambao ni madaktari bingwa wa upasuaji watoto, upasuaji rekebishi, usingizi na ganzi, watalaam wa lishe pamoja na radiolojia.
“Tuliwapokea watoto hawa Machi 11 2023, wakiwa na jumla ya kilo nne hivyo tulianza mchakato wa kuwahusisha wataalam ambao wanahusika na huduma hizi, ilituchukua takribani muda wa miezi kumi kuangalia mwenendo wao wa afya kwa ujumla kabla ya kuwatenganisha ili kuweza kupata dira ya namna watakavyoishi mara baada ya kutenganishwa, ” amesema Ngota.
Amesema hadi pacha hao wanatenganishwa walikua na kilo 16 sawa na kilo nane kwa kila mmoja.
Aidha, mzazi wa watoto hawa, Mariam Shabani, mkazi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam, ameishukuru serikali na watoa huduma wote wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na jinsi alivyohudumiwa katika kipindi chote alichokuwa hapo.