India yatuhumiwa kutaka kuishambulia Pakistan

ISLAMABAD: SERIKALI ya Pakistan imedai kuwa ina ushahidi wa kijasusi na wa kuaminika unaoonesha kuwa India inapanga kuishambulia katika muda mfupi ujao.
Tuhuma hizo zimeibuka wakati raia wa Pakistan wanaoishi India wakianza kurejea nyumbani kufuatia amri ya serikali ya India ya kuwataka kuondoka, baada ya tukio la shambulio katika jimbo la Kashmir wiki iliyopita.
Mashambulio dhidi ya watalii katika jimbo hilo na hatua ya India kuituhumu Pakistan kuwa inahusika na tukio hilo jambo ambalo Pakistan imekanusha vikali vimeongeza mvutano mkubwa kati ya mataifa hayo hasimu yenye silaha za nyuklia.
Mvutano huo sasa unatajwa kuwa mkubwa zaidi tangu mwaka 2019.Pakistan imeeleza kuwa ina taarifa za ndani zinazoonesha kuwa ndani ya saa 24 hadi 36, India huenda ikafanya mashambulizi ya kijeshi kwa madai ya uwongo kuwa Pakistan inahusika na mashambulio ya kigaidi katika eneo la Pahalgam.
Hadi sasa, India haijatoa tamko lolote rasmi kuhusu tuhuma hizo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amewasiliana kwa njia ya simu na viongozi wa India na Pakistan, akisisitiza umuhimu wa pande hizo mbili kuepusha mvutano unaoweza kusababisha athari kubwa kwa usalama wa kikanda.
SOMA: Ubalozi India kupokea wageni tuzo za uchoraji