PANYA Buku waliopata mafunzo katika Chuo cha Sua wanatumika kutambua sampuli zaidi ya 100 kwa dakika 20 za vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu.
Panya hao wanaopatikana kwenye maabara za APOPO Dar es Salaam na SUA Morogoro huweza kutambua vimelea vya TB kwenye makohozi kwa kasi kubwa kiasi kuliko wataalamu wa maabara ambao wanatumia siku nne kuchunguza idadi hiyo ya sampuli.
APOPO hukusanya sampuli kutoka kwenye vituo vinavyopima TB kwa ajili ya mafunzo kwa Panya lakini pia kwa utambuzi zaidi ili kubaini uwepo wa vimelea hivyo vya TB.
Akizungumza na HabariLeo, Mratibu wa Kifua Kikuu, Mkoa wa Dar es Salama Mbarouk Seif Khaleif amesema Panya hao hupewa mafunzo na wana uwezo wa kunusa na kutambua kwa haraka vimelea vya ugonjwa wa TB.
“Sampuli zinapangwa nyingi hapo, panya anapita kufanya utambuzi, anaponusa sampuli ya makohozi iliyo na vimelea huonyesha ishara ya kuchakura eneo hiyo kuashiria kuna vimelea vya TB na hapo sisi tunachukua hiyo sampuli na ukiipeleka maabara kwa uhakiki kweli utakuta ni TB.”Amesema
Mfumo huu wa kutumia panya kutambua TB ulianzishwa na shirika la misaada Ubelgiji, kama njia nyepesi na na isiyotumia fedha nyingi kutambua TB kinyume na mfumo uliozoeleka.
Kwa mujibu wa Dk Mbarouk anasema Dar es Salaam ndio inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi wa TB huku, takwimu za Wizara ya Afya zilizotolewa Machi 24 na Waziri Ummy Mwalimu zinaonyesha kuwa watu 71 ufariki kila siku nchini kutokana na ugonjwa wa TB.