Papa Leo XIV mwenyeji Tanzania

VIONGOZI wa Kanisa Katoliki wamethibitisha kwamba, Papa Leo XIV si mgeni nchini baada ya kukanyaga ardhi hiyo akiwa Mkuu wa Shirika la Mtakatifu Augustino duniani.
Papa Leo XIV ambaye anasifika kwa kuwa kiongozi anayesikiliza watu na rahisi kufikika kwa wote wanaomuhitaji, kwa miaka tofauti aliwahi kufika Tanzania na kupita maeneo kadhaa ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Njombe na katika nyumba ya malezi ya shirika hilo iliyopo Mahanje Jimbo Kuu Katoliki la Songea.
Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za pongezi kwa Papa Leo XIV kwa kuchaguliwa kuongoza Kanisa Katoliki duniani.
Alisema: “Kwa niaba ya serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nakutakia kila la heri katika utumishi wako kwa kanisa na dunia kwa ujumla nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akusimamie na kukuongoza”.
Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Stephano Musomba ambaye ni mwanashirika wa Mtakatifu Augustino (O.S.A), alisema kwa mara ya kwanza alimuona Papa Leo XIV nchini mwaka 2003 alipokuwa mkuu wa shirika hilo.
Alisema kwa jinsi alivyokaa nae na kuzungumza naye ana kwa ana, ana matumaini makubwa katika uongozi wake na katika yote atakayoyafanya.
“Papa Leo XIV alikuja Tanzania mwaka 2003, kutembelea jumuiya za Waagustino Tanzania yeye akiwa mkuu wa shirika ulimwenguni. Na kati ya shughuli alizozifanya, alikuja akafikia kwenye nyumba yetu ya Mahanje kule Songea,” alisema Askofu Musomba.
Alisema kama mkuu wa shirika alikuwa na wajibu wa kutembelea jumuiya zote za shirika hilo na kwa Tanzania walikuwa na nyumba ya malezi huko Mahanje, Songea mkoani Ruvuma, Morogoro na Parokia ya Mavurunza, Jimbo Kuu la Dar es Salaam.
Alieleza: “Sijajua kama alifika Dar es Salaam, wakati huo tuna Parokia ya Mavurunza, baadaye kuna nyumba ya malezi pale Morogoro bila shaka alipita kote huko na ndiyo baadaye akaja kule Kusini Songea katika jumuiya yetu iliyoko Mahanje”.
Askofu Musomba anasimulia wakati alipofika kwenye nyumba hiyo ya malezi, alitembelea na sehemu nyingine na aliporudi alimkuta akiwa bado Songea.
“Tulipanda gari moja na Papa Leo (akiwa mkuu wa shirika) na mimi ndiye niliendesha gari kutoka Songea mpaka Morogoro na Agosti 28, 2003 alipokea nadhiri za daima za watawa wao watatu,” alifafanua.
Akizungumzia aina yake ya uongozi, Askofu Musomba alisema: “Ni mtu ambaye anafikika yaani ni rahisi kumfikia si mtu wa vitisho, ni kiongozi ambaye anasikiliza na mtu ambaye unakuwa huru kuongea naye.”
Pia, alisema anamuona kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani kama baba ambaye anaongea na mwana na anamsikiliza anasema nini na kwamba walikuwa huru kuzungumza naye walipokuwa na shida fulani.
“Nilipoenda Ulaya kusoma nilikaa naye Roma kule kwenye nyumba yetu ya makao makuu ya shirika nilipokuwa nasoma Chuo cha Augustino nilikaa naye miaka minne kuanzia mwaka 2004 hadi 2008,” alisisitiza.
Akielezea kuhusu Shirika la Mtakatifu Augustino, Askofu Musomba alisema ni shirika kongwe lililoanzishwa mwaka 1256 na kwamba maisha wanayoyaishi kama Waagustino yameanzishwa na Mtakatifu Augustino.
Alisema shirika limeanzishwa na kanisa lenyewe mwaka 1444 na Papa Alexander IV ndiye aliyelitambulisha maana kulikuwa na vikundi vilivyokuwa vinaishi maisha ya Waagustino lakini aliona ni vema waishi kama shirika.
Alisema katika shirika hilo, watawa hufunga nadhiri tatu ambazo ni mashauri ya injili, ufukara, utii na useja.
Kwa upande wake, Katibu wa Shirika La Agustino Vikarieti ya Tanzania na Paroko wa Mavurunza, Padri Urick Kinyero alisema Papa Leo XIV aliwahi kufika Tanzania kwa nyakati tofauti na kupita Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Njombe, Ruvuma, Madaba katika Kijiji cha Mahanje jimboni Songea ambako shirika lilianzia mwaka 1978.
“Ni furaha kwetu kwa kuwa amekanyaga ardhi ya Tanzania, tulisalimiana naye na kukaa naye kwenye vikao, kila nyumba aliongea na watawa mmojammoja, walezi na wanafunzi waliofunga nadhiri na mimi niliongea naye,” alisema.
“Alikaa kama siku mbili au tatu, tulikula wote na tulisali wote. Wakati huo, alitutaka tujitahidi kusoma, kupata malezi vizuri ya Kiagustino, kulijua shirika na kanisa vizuri,” alisisitiza.
Pia, alisema alikula vyakula walivyokula wao, hakubagua na walikula pamoja naye mezani kama kawaida.
Kwa upande wa Familia ya Shirika la Mtakatifu Augustino Mkoa wa Morogoro wamemtaja, Papa Leo XIV ambaye aliwahi kufika Morogoro akiwa mkuu wa shirika hilo duniani, kuwa ni mpenda amani, mwenye kupenda watu, kuwaheshimu, amani, haki na kutendeana haki wenyewe kwa wenyewe.
Mkuu wa Nyumba ya Mtakatifu Augustino, Padri Ephrem Msigala alisema wanamfahamu, Papa Leo XIV kwa jina lake la Robert Francis Prevost (O.S.A) alipokuwa mkuu wa shirika hilo duniani baada ya kufika mkoani Morogoro mwaka 2003.
“Kwenye nyumba ya shirika alipita kwa muda na hakukaa muda mrefu kwani ni kama siku tatu na aliondoka kuendelea na safari maeneo mengine,” alisema.
Padri Msigala alimtaja ni mtu anayependa kuunganisha watu na atakuwa ni mpatamishi katika nchi zenye ugomvi na hali ya kutoelewana.
Alisema wao wanaamini kwa nafasi aliyochaguliwa ni sahihi kwa kuwa anao upeo kwani aliangalia katika historia yake alichaguliwa kama mkuu wa Jimbo la Augustino mwaka 1999 na mwaka 2001 aliteuliwa kuwa mkuu wa shirika hilo duniani.
Padri Msigala alisema aliongoza shirika hilo duniani kwa vipindi viwili na kumaliza mwaka 2013 na baada ya hapo alirudi kwao Chicago, Marekani.
Alisema lakini hakukaa muda mrefu kwani Papa Francis alimteua kuwa Askofu wa Chiclayo nchini Peru, Amerika ya Kusini na kudumu mwaka 2015 hadi kufikia mwaka 2023.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button