Pazia fomu uteuzi urais kufungwa leo

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) leo inatarajiwa kukamilisha kazi ya kuwapa fomu za uteuzi wagombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Hadi sasa Mwenyetiki wa INEC Jaji wa Rufaa, Jacobs Mwambegele amekabidhi fomu kwa wagombea wa
vyama 15.
Kati ya hao wagombea, wanawake wawili wanawania kugombea urais na wengine wanane ni wagombea wenza.
Wengi wa wagombea hao wametaja vipaumbele vya ajira kwa vijana, kilimo, elimu, afya na mabadiliko ya katiba.
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan alikuwa wa kwanza kuchukua fomu hizo Agosti 9 katika ofisi za INEC Dodoma.
Rais Samia alisema chama kimejipanga kutekeleza ilani yake na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuimarisha uchumi wa viwanda, kilimo cha kisasa, ajira kwa vijana na wanawake pamoja na afya bora kwa wote.
“Tangu 2021 hadi 2025, hakuna sekta ambayo hatukuigusa, mafanikio hayo yapo dhahiri… niwahakikishie
katika miaka mitano ijayo, tutakapoanza utekelezaji wa dira ya taifa 2050 (Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050) tutafanya makubwa zaidi,” alisema.
NRA
Mgombea urais kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Kisabya alisema chama hicho hakipo tayari kuliingiza Taifa katika machafuko kwa kisingizio cha uchaguzi.
AAFP
Mgombea urais kupitia Chama cha Wakulima (AAFP), Kunje Ngombale Mwilu alisema serikali itahamasisha uzalendo.
MAKINI
Mgombea urais kupitia Chama cha MAKINI, Coaster Kibonde alisema chama hicho kimejipanga kutekeleza ajenda za elimu, kilimo na afya.
NLD
Mgombea wa urais kupitia Chama cha The National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo alisema vipaumbele vya chama hicho ni ajira, afya, elimu, miundombinu na haki.
UPDP
Mgombe wa Chama cha United Peoples’ Democratic Party (UPDP), Twalib Kadege alisema sera ya chama hicho ni ardhi kwa kuwa ndiyo msingi wa maisha ya kila kiumbe.
ADA-TADEA
Mgombea wa kiti cha urais kupitia Chama cha African Democratic Alliance Party (ADA – TADEA), Georges Bussungu alisema serikali yake italeta mapinduzi ya njano ambayo ni ya fikra, teknolojia inayojikita katika akili unde na uchumi.
UMD
Mgombea urais kupitia Chama cha Union for Multiparty Democracy (UMD), Mwajuma Mirambo alisema chama hicho kinaamini katika sera ya majimbo, kina sera wezeshi na rafiki kwa kila Mtanzania.
TLP
Mgombea wa urais kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira alisema vipaumbele vya chama hicho ni ulinzi na usalama wa nchi, utawala bora na uchumi imara.
CCK
Mgombea urais kupitia Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele alisema CCK imejipanga kuleta mageuzi katika sekta za maendeleo nchini kikiwemo kilimo cha kisasa, elimu, afya, ajira pamoja na ustawi wa jamii.
CHAUMMA
Mgombea wa urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu alisema ilani ya chama hicho imezingatia nguzo kuu nane zenye dhumuni la kuleta maendeleo ya kiuchumi yatakayomwezesha
Mtanzania kuondokana na umasikini wa kipato.
DP
Mgombea wa urais kupitia Chama cha Democratic Party (DP), Abdul Juma Mluya alisema serikali yake itaboresha huduma za afya kwa wajawazito, kilimo na masilahi ya watumishi wa umma.
SAU
Mgombea urais kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara alisema chama hicho kitaunda serikali ya watu wenye hofu ya Mungu, wenye uzalendo, uadilifu na wenye kutenda haki.
CUF
Mgombea urais kupitia Chama cha The Civic United Front (CUF), Gombo Samandito Gombo alisema chama hicho kitaendelea na msimamo wa kuhakikisha kuna haki sawa kwa wote.


