‘Pelekeni watoto haraka kutibiwa saratani ya macho’

DAKTARI bingwa wa magonjwa ya macho Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke, Annamary Stanslaus amesema ili kupunguza vifo vitokanavyo na saratani ya macho ya watoto ‘Retinoblastoma’,  wazazi na walezi hawana budi  kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya afya mara tu wanapoona dalili zisizo za kawaida katika macho ya mtoto.

Kauli hiyo ameitoa leo Mei 19, 2023 Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke katika maadhimisho ya wiki ya kuelimisha saratani ya macho kwa watoto.

Advertisement

“Takribani asilimia 70 hadi 90 ya watoto hawa hufika kwenye hospitali za rufaa za kanda wakiwa kwenye hatua kubwa za magonjwa. Hali hii husababisha asilimia 50 hadi 70 kupoteza maisha kwa sababu ya kuchelewa kupatiwa huduma,”  amesema.

Akitoa elimu kuhusu ugonjwa huo, Mratibu huduma ya macho manispaa ya Temeke Dk Daniel Ringo ameelezea maana ya Retinoblastoma kuwa ni ugonjwa unaojitokeza kwenye jicho moja au yote mawili na inatokana na vinasaba kwenye utando au pazia la ufahamu la jicho linaloitwa kwa kitaalamu retina.

“Hitilafu hii inaweza kuwa na historia ya ugonjwa kwenye familia. Ni muhimu kwa wanafamilia wa karibu na watoto wao kuangaliwa pia pindi inapotokea kwenye familia amepatikana na ugonjwa huu,” amesema.

Dk Ringo ameongeza kuwa saratani hii hujitokeza zaidi katika miaka mitano ya mwanzo tangu kuzaliwa. Mara chache sana kujitokeza baada ya miaka 5. Vilevile saratani hii huwapata watoto wote wa jinsia ya kiume na kike.

“Dalili za Saratani ya macho kwa watoto huwa zinafanana na zimegawanyika katika dalili za awali na zilizokomaa,” amesema.

Alizitaja dalili za awali kuwa ni i) Weupe kwenye mboni ii) Jicho kung’aa wakati wa jioni na asubuhi iii) Kengeza iv) Jicho kuvilia damu, kuwa jekundu, kubadilika rangi au kuuma v) weusi wa jicho kubadilika rangi na vi) kupoteza uwezo wa kuona.

Alizitaja dalili zilizokomaa ni i) jicho kuwa kubwa ii) jicho kuvimba na kutokeza nje na iii) kidonda kwenye jicho au macho.

Kwa upande wake Meneja Miradi Sense International, Lisa Mungure amesema wao kama wawezeshaji watakuwa bega kwa bega katika mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo na mengine hatarishi.

/* */