Polepole kumwandikia Rais Samia wasiotumia dawa viuadudu Kibaha

MALARIA ni moja ya ugonjwa unaoongoza kuua ikiwemo wajawazito na watoto wachanga nchini. Asilimia 36 ya vifo vinatokana na ugonjwa huo.

Hata hivyo, jitihada za kuutokomeza zilianza tangu mwaka 1901 kukiwa na kampeni zenye nia thabiti ya kuhakikisha lengo linafikiwa la kuiwezesha Tanzania kuwa salama bila kuwa na ugonjwa huo.

Mbali ya kampeni mbalimbali pamoja na jitihada zilizochukuliwa lakini bado kiwango cha ugonjwa huo kimeendelea kuongezeka badala ya kupungua kama ilivyodhamiriwa.

Meneja Udhibiti Ubora katika kiwanda cha kibayoteknolojia cha kuua viuadudu vya malaria (TBPL) kilichoko Kibaha mkoani Pwani, Samuel Mziray anasema kuanzia mwaka 1901 kulikuwa na kampeni ya usafi wa mazingira na kufukia mashimo yanayoweza kuwa chanzo cha mazalia ya mbu.

Anasema mwaka 1913 ilianzishwa sheria ya mbu kuuawa na mwaka 1921 ikaelezwa kuwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo aripoti kituo cha afya na mwaka 1922 vyandarua viliingia lakini kwa wenye asili nyeupe na katika mwaka 1930 vilianzishwa vikundi vya vijana kuzibua mifereji ili kuondoa mazalia ya viluwiluwi vya mbu na kufikia mwaka 1950 dunia iligundua kemikali za kupambana na mbu ikiwemo kemikali ya DDT.

Mziray anasema DDT iligundulika kuua kiumbe yoyote aliyeko kwenye mazingira na ina uwezo wa kukaa kwa miaka 70 kabla ya nguvu yake kuisha na kutokana na kutokuwa rafiki wa afya wala mazingira mwaka 1970 ilipigwa marufuku.

Aidha, anasema kwa Tanzania baadhi waliitumia kupaka katika kuta na hata kutumika kama viuadudu hadi mwaka 1988 kampeni ya malaria ilianzishwa na mwaka 1990 kilianzishwa kitengo cha kupambana na malaria.

Mziray anasema mwaka 2007 Mawaziri wa Afya wa Afrika waliazimia ifikapo mwaka 2030 malaria imalizike na kuanzia mwaka 2010, chini ya uongozi wa awamu ya nne, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete Tanzania iliazimia kujenga kiwanda cha kibayoteknolojia kilichoko Kibaha mkoani Pwani.

Kiwanda hicho kimejengwa kwa ushirikiano na serikali ya Cuba, ambapo ni cha tatu duniani, kimoja kikiwa Cuba, kingine Japan na Tanzania lengo likiwa ni kupambana na ugonjwa wa malaria ambao umekuwa ukiathiri walio wengi.

Kiwanda hicho kwa sasa kinazalisha bidhaa za kibayoteknolojia zenye kuua bakteria na wadudu mbalimbali wakiwemo viluwiluwi wanaozalisha mbu lakini haina madhara kimazingira na hata kiafya.

Kiwanda hicho kinachoratibiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kinazalisha dawa ya kuua viuadudu vya malaria lengo lake ni kutokomeza mbu na ugonjwa wa malaria nchini.

Anasema matumizi ya dawa ya viuadudu huweza kuua wadudu kwa asilimia 100 ndani ya saa 24.

Uanzishwaji wa kiwanda hicho ulilenga kumaliza malaria ifikapo 2025 lakini takwimu zimeendelea kuonesha kuwa badala ya kiwango kushuka ama kuisha, kimezidi kuongezeka hivyo ipo shida katika matumizi ya dawa hiyo kwenye maeneo maji yanapotuama ambapo ndipo mazalia ya mbu.

Kiwanda hicho kinazalisha dawa za mfumo wa kimiminika ambazo zimehifadhiwa kwa ujazo mbalimbali na zikitumika ipasavyo zina uwezo wa kuharibu mazalia ya mbu katika maeneo mbalimbali.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa kiwanda hicho chini ya NDC, Dk Nicholas Shombe, anasema mbali ya dawa ya viuadudu, kiwanda kina uwezo wa kuzalisha bidhaa nyingine kama dawa ya kuulia wadudu kwenye mazao ya mahindi, pamba na mbogamboga.

Vilevile wana uwezo wa kuzalisha chanjo mbalimbali na mbolea vyote vikiwa ni rafiki kwa afya na mazingira.

Ni kiwanda ambacho kinatumika kama shule na maabara pia ambayo husaidia kufundisha kuhusu baiyoteknolojia. Kuwepo kwa kiwanda hicho nchini ni alama kubwa ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Cuba.

Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha dawa lita milioni sita na mchango wake kwenye malaria ni mkubwa pamoja na kutokomeza magonjwa kama Dengue. Mpaka sasa ni lita 400,000 tu zilizonunuliwa.

Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole alipotembelea kiwando hicho hivi karibuni, aliwataka viongozi nchini kuwa na hekima na huruma na kuhakikisha katika bajeti ya fedha ijayo ya mwaka 2023/24 wanatenga fedha ili kununua dawa ya kuulia viuadudu vya malaria na ziwafikie wananchi.

Polepole anasema kila baada ya miezi miwili atakuwa akiwaandika hadharani lakini pia kumwandikia Rais Samia Suluhu Hassan mikoa ambayo haijakwenda kununua dawa hiyo TBPL.

Anasema kwa kila mwenye dhamana ya serikali na hafiki kiwandani hapo kununua dawa ya kuua viuadudu vya malaria kama asipokuwa mhuni atakuwa muuaji.

Licha ya kiwanda hicho cha kipekee kujengwa nchini lakini kiwango cha malaria kimeendelea kuongezeka na hali hiyo inaonesha kutozingatiwa sababu ya ujenzi wa kiwanda hicho.

“Nikiwa kama Balozi yapo mengi ya kwenda kueleza huko Cuba…nawaombea kwa Mungu viongozi wetu wanapokamilisha bajeti ya fedha ya 2023/24 kutenga fedha ili kununua dawa hizo na ziwafikie wananchi,” alisema Polepole na kueleza hakuna sababu ya kuwa na malaria Tanzania.

Anasema kiwanda kilijengwa tangu mwaka 2016 kwa nia njema ya kuokoa maisha ya Watanzania na kuzinduliwa mwaka 2017.

Anasema licha ya maelekezo mengi kutolewa na viongozi kwa Wizara ya Afya, Tamisemi na katika halmashauri zote nchini za kununua dawa hiyo ili kupuliza maeneo yao lakini hakuna hatua muhimu zilizochukuliwa.

Anasema baada ya kuzinduliwa kwa kiwanda hicho, ilitarajiwa hadi mwaka 2022 malaria nchini iwe imetokomezwa lakini mkazo wa jambo hilo haujawekwa.

“Malaria kuwepo nchini ni uamuzi wetu, Wizara ya Afya, Tamisemi na halmashauri nani ana jeuri ya kutonunua dawa hizo…ninakwenda Cuba kuomba ushirikiano, nitapata wapi uhalali kama hata katika hili tumelitelekeza?” Amehoji Polepole na kuongeza ikifika Agosti atauliza mikoa na halmashauri zilizofika na kununua dawa.

Mtwara inaongoza kwa kiwango cha malaria kwa asilimia 20, Tabora 23, Kagera 18, Mara 15 na Geita 13 hapa lazima kununua dawa mpende msipende.

Polepole anasema iwapo malaria itakwisha, kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha bidhaa nyingine ikiwemo dawa ya kuulia wadudu katika mazao. Anashangaa kuona wanazungushwa kupata kibali ili dawa hiyo iingie sokoni na kuahidi wasipopewa atamuandikia Rais Samia.

Naye Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Yordenis Despaigne, alisema kiwanda hicho kwa Tanzania ni muhimu na faida zake zitaonekana kwa kutokomeza malaria.

Habari Zifananazo

Back to top button