Polisi Arusha waja na mbinu mpya kushughulikia wahalifu

ARUSHA: Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limekuja na mbinu mpya ya kukabiliana na matukio ya uhalifu katika mkoa huo ambapo wamewapanga askari katika mitaa yote ambayo watashirikiana na wananchi wa mitaa husika ili kutatua changamoto mbalimbali za uhalifu.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kamishna msaidizi wa Polisi ACP, Justine Masejo katika Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha wakati akizindua mpango wa ulinzi ambao umeanzishwa na Jeshi Polisi mkoani humo ambapo kila mtaa utakua na Askari Polisi ambaye atakua na jukumu la kusikiliza na kutatua changamoto za kiusalama.

ACP Masejo amebainisha kuwa mpango huo umekuja baada ya mpango wa Polisi Kata kuwa na matokeo chanya, hivyo Jeshi hilo limeona vyema kuja na mpango huo wa ulinzi katika mitaa ambao utasaidia kusogeza huduma za kipolisi hadi kuanzia ngazi za chini.

Aidha ameendelea kufafanua kuwa mpango huo utasaidia kuimarisha ulinzi wa wananchi pamoja na watalii wanaofika  mkoa huo ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini na wengine wao hutembelea na kuishi katika mitaa mbalimbali kupitia programu ya makazi mtandaoni maarufu ‘‘air bnb’’.

Kwa upande wake Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Arusha kamishna msaidizi wa Polisi ACP, Peter Lusesa amebainisha kuwa tayari Kamisheni hiyo ngazi ya mkoa imeshatoa mafunzo kwa askari wanaokwenda kutoa huduma katika mitaa mbalimbali ya Mkoa wa Arusha.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button