Polisi Iringa wanolewa udereva
MAOFISA 123 wa jeshi la polisi Mkoa wa Iringa wamepata mafunzo maalum ya udereva kama moja ya mkakati wa jeshi hilo kuwaongezea askari hao ujuzi utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo pamoja na kushughulikia makosa ya barabarani na dharula.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yametolewa na Chuo cha Ufundi Stadi (Veta) Iringa yakihusu udereva wa kujilinda, mbinu za kufuatilia, na kushughulikia dharula, usalama na ajali zote za barabarani.
Mratibu wa mafunzo ya muda mfupi wa chuo hicho, Edmund Enugu alisema askari hao wamefundishwa pia falsafa ya udereva inayolenga kuelewa na kutafakari kuhusu maana, umuhimu, na misingi ya udereva.
“Falsafa hii inahusisha mawazo na maadili yanayohusiana na kuwa dereva kama taaluma kamili pamoja na jukumu la kibinafsi na kijamii katika kutumia barabara,” alisema.
Enugu alizungumzia pia jinsi mafunzo hayo yalivyowaongezea uelewa askari hao kuhusu umri mdogo wa dereva na namna unavyoweza kuwa sababu ya ajali za barabarani.
Alisema madereva vijana wanaweza kukabiliwa na changamoto kama uzoefu mdogo wa kuendesha, upungufu wa tahadhari, na tabia ya kutokuwa na utulivu barabarani.
Awali Mkuu wa chuo hicho, Pasiens Nyoni aliwapongeza askari hao akisema pamoja uzoefu wa jukumu lao la kushughulikia makosa na ajali za barabarani wameamua kujinoa zaidi ile wawe wajuzi bora katika kushughulikia makosa ya barabarani kwa kuzingatia pia matumizi ya teknolojia zinazokua siku hadi siku.
Alisema ukuaji wa teknolojia umesaidia sana katika kudhibiti makosa ya barabarani na akatoa mifano kuwa ni pamoja na matumizi ya kamera za usalama na mfumo wa kielektroniki wa kuangalia mwendo wa gari ambao umesaidia kuongeza usalama barabarani na kupunguza ajali zinazotokana na makosa ya madereva.
Kwa kupitia mafunzo hayo Nyoni alisema maafisa 99 wapata ufaulu utakaowawezesha kupata leseni daraja D, saba daraja C1, mmoja daraja C na 16 daraja E.
Akikabidhi vyeti vya kuhitimu mafunzo hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi alisema ili jeshi la Polisi liweze kusimamia sheria na kutekeleza majukumu yake ipasavyo limeendelea kufanya uhakiki wa leseni za udereva kwa askari wenye sifa stahiki.
Alisema jeshi lake limeamua kuwaongezea ujuzi wale wasio na leseni ili waweze kuzimiliki kama sifa ya kuwa askari mahiri kwenye fani ya udereva wa vyombo vya moto.
“Na kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaboresha utendaji wa jumla wa fani ya udereva katika kudhibiti ajali za mtu mmoja mmoja, makundi na taasisi za serikali,” alisema.
Aidha alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa linatarajia kuingia awamu ya pili ya mafunzo kwa watumishi wa taasisi za serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwa wameazimia kuboresha fani ya udereva na kudhibiti vyanzo vya ajali vinavyosababishwa na madereva wasio na sifa.
Alisema jeshi hilo linatarajia kuinua fani ya udereva kama fani nyingine badala ya kuichukulia kama fani mbadala kwa kukosa ajira au kimbilio la walio kwenye maisha magumu.