POLISI mkoani Kigoma wametakiwa kuacha tabia ya kutumia nguvu ikiwemo kuwachapa fimbo waendesha pikipiki maarufu bodaboda wanapofanya makosa barabarani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa Kigoma, Abdulkadri Mushi amesema hayo mjini Kigoma katika kikao cha kuzungumzia vurugu zinazoendelea baina ya pande hizo mbili ambapo aliwataka polisi kuacha kukamata watuhumiwa wa makosa ya usalama barabarani kwa kutumia taratibu ambazo hazipo kisheria
Sambamba na hilo amewataka waendesha pikipiki hao kufuata taratibu za usalama barabarani ikiwemo kukamilisha taratibu za vyombo vya moto, kuwa na saiti mila kwenye pikipiki, kuvaa kofia ngumu, kukubali kukamatwa bila shuruti na kufikishwa kituoni wanapotuhumiwa kuwa na makosa na kwamba hiyo yote itaondoa vurugu hizo.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Waendesha Bodaboda Kigoma, Samwel Mtema amesema kuwa tangu kuanza kwa operesheni ya kukamata makosa ya usalama barabarani kwa bodaboda Desemba 16 mwaka huu vurugu imekuwa kubwa na hakuna mahusiano mazuri baina ya polisi na bodaboda kwa sababu ya polisi kutumia nguvu ikiwemo kuwachapa fimbo bodaboda hivyo kuwepo kwa matukio ya kupigana baina ya pande hizo mbili yanayoendelea katika wilaya zote za mkoa Kigoma.
Akitoa ufafanuzi kuhusu operesheni hiyo Mkuu wa Dawati la Polisi Jamii Kigoma, Juma Majula amesema kuwa ni operesheni inayofanyika nchi nzima kwa maelekezo ya mkuu wa jeshi la polisi nchini na kwamba changamoto za vurugu zinazotokea zinatokana na baadhi ya bodaboda kupinga kukamatwa au kupinga kuchukuliwa pikipiki zao zinapokutwa na makosa.
Hata hivyo Majula amesema kuwa kama kuna changamoto zinazojitokeza katika operesheni hiyo inatokana na hali ya kibindamu ya baadhi ya watendaji hao wa polisi na hivyo baada ya kikao hicho watafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa ili zoezi hilo linalopaswa kukamilika Desemba 31 mwaka huu liweze kuendelea kwa kufuata sheria na taratibu za nchi zilizowekwa.