Polisi yadaka 11 wale ‘Tuma kwa namba hii’

JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga, limekamata watu 11, wakiwemo wanawake wawili na wanaume tisa wakazi wa Dar es Salaam, wakituhumiwa kujihusisha na wizi wa fedha kwa njia ya simu.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutuma ujumbe kwa watu mbalimbali wakiwataka wawatumie fedha, baadhi ya ujumbe wanaotuma ni: ‘Nitumie kwa Namba hii, au Tuma kwa namba hii.’

Ujumbe mwingine wanaotumia ni: “Mimi mwenye nyumba wako, ile pesa nitumie kwa namba hii’.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe amesema kuwa watuhumiwa wote walikuwa wakiishi katika nyumba moja waliyokuwa wamepanga maeneo ya Donge, Kata ya Mnyanjani jijini Tanga.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na vitu mbalimbali ikiwemo laini za simu 441, karatasi 43 zilizoandikwa namba za simu na namba za mawakala wa mitandao ya fedha, kadi tano za benki mbalimbali, vitambulisho 14, na betri za simu ndogo 7.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 11, ambao wanajihusisha na uhalifu kwa njia ya mtandao, ambao hutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa watu mbalimbali wakiwataka watume pesa, baada ya kukamatwa walikutwa na fedha taslimu Sh 2,085,000, pesa ya Congo 450,100, simu kubwa 11, simu ndogo 13, kadi 5 za benki mbalimbali, ” amesema.

“Aidha katika ufuatiliaji jumla ya laini za simu 441 walizokuwa nazo watuhumiwa kwa lengo la kuwatapeli watu mbalimbali kwa kuziorodhesha namba za simu na majina ya watumiaji, laini 399 za simu baada ya kufanya utapeli walizichoma moto na kati ya laini hizo 183 zilitumiwa ujumbe mfupi wa maneno na kumtaka mwananchi atume pesa.

“Laini 42 za simu zilikuwa katika mchakato wa kuwatapeli watu mbalimbali, watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayowakabili, ” amesema Kamanda Mwaibambe.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button