JESHI la Polisi mkoani Kagera limewaua watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika Kijiji cha Kumunazi wilayani Ngara mkoani Kagera.
–
Kamanda wa Polisi Mkoa Kagera, William Mwampaghale, amesema watuhumiwa hao wanakadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 na 30, lakini majina yao bado hayajatambulika, ila miili imehifadhiwa Hospital ya Rufaa ya Nyamihaga wilayani Ngara.
–
Alisema Januari 21, 2023, polisi ilipata taarifa kuuna kundi la wahalifu wanaotumia pikipiki linapanga kufanya uhalifu Kati ya barabaraba ya Kumunazi na Rulenge, ambapo majira ya saa 3;35 polisi liliweka mitego mbalimbali na kufanikiwa kunasa wahalifu hao, ambao walikufa katika kurushiana risasi.
–
” Katika mtego wetu ilipita pikipiki tuliyoihofia ambayo ilikuwa imebeba watu watatu ,polisi waliisimamisha pikipiki hiyo lakini haikusimama, wakafyatua risasi juu, lakini bado waliendelea kukimbia,” alisema.
Alisema waliwakimbiza lakini walikaidi na kuanza kurushiana risasi, ambapo mmoja alijeruhiwa mguuni na mwingine kiunoni na hali zao zilikuwa mbaya wakati wakikimbizwa Hospital ya Nyamihaga.
–
Alisema mara baada ya kufanya upekuzi kwenye makoti waliyokuwa wamevaa, walikutwa wakiwa wamebeba bunduki aina ya AK47, ikiwa na risasi 25 pamoja na mabomu 2 ya kurusha kwa mkono.