Polisi yawarudisha shuleni wanafunzi watoro Lindi

LINDI: MKAGUZI Msaidizi wa Polisi wa Kata ya Majengo, Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Marwa Benedict, kwa kushirikiana na viongozi wa kata na kijiji, ameongoza zoezi la kuwarudisha shuleni wanafunzi watoro wa shule za msingi katika kata hiyo.
Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu stahiki na kuepuka madhara yanayotokana na utoro wa shuleni. Katika zoezi hilo, Marwa aliwapatia wanafunzi hao elimu kuhusu madhara ya kuacha shule, huku akiwahimiza kutambua umuhimu wa kusoma kwa maendeleo yao ya baadaye.
Alisisitiza kuwa elimu ni msingi wa maisha bora na huwasaidia watoto kujijengea mustakabali mzuri.
Baada ya kupewa elimu hiyo, wanafunzi wote waliokuwa watoro wameahidi kurudi shuleni na kuendelea na masomo yao. Wameeleza kuwa awali hawakuelewa thamani ya elimu, lakini sasa wanafahamu umuhimu wake na wamejipanga kutotoroka tena.
Kwa upande wa wazazi, baada ya kupata elimu juu ya umuhimu wa kusimamia masomo ya watoto wao, wameahidi kushirikiana na walimu kwa karibu na wamekubali kuwa bega kwa bega na walimu ili kuhakikisha watoto wao wanapata maendeleo chanya katika masomo yao na kuondokana na utoro.



