Pombe, sheria na ukatili kwa watoto kizungumkuti

“Ndiyo. Pombe inaweza kuwa aina ya ukatili kwa watoto, si tu kwa kuwanyima malezi bora, bali pia kwa kuwaweka katika mazingira hatarishi,” anasema mraghibishi Jelda Laurent.
Laurent anayefanya kazi ya kujitolea na Kituo cha Taarifa na Maarifa ya Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia, kinachofanya kazi na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Katika kata ya Kalenga anasema ukatili wa kimwili, kingono, na kihisia unaochangiwa na pombe unaathiri maisha ya watoto.
Katika kata hiyo ya Kalenga iliyopo wilayani Iringa, mkoani Iringa anasema baadhi ya watoto wanakua katika mazingira ambayo pombe imekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Katika mkutano uliowakutanisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Kalenga kujadili masuala ya ukatili ikiwa ni pamoja na sheria na madhara ya pombe kwa watoto, Laurent ameweka hoja yake mezani:
“Je, watoto wa Kalenga na maeneo mengine ya Tanzania wanalindwa kweli dhidi ya madhara ya pombe, na je, sheria zilizopo zinachangia au kupunguza ukatili dhidi ya watoto?
Mraghibishi huyo anasema watoto wanaokulia katika nyumba zinazouza pombe au karibu na baa wanakumbana na aina mbalimbali za ukatili.
Akizungumzia ukatili wa kimwili anasema walevi wanaweza kuwapiga au kuwafanyia vitendo vya unyanyasaji watoto.

Na kwa ukatili wa kingono anasema watoto wa kike wako hatarini kutumiwa vibaya na watu waliopoteza udhibiti kutokana na pombe.
Kuhusu ukatili wa kihisia anasema watoto wanakua katika mazingira yasiyo salama kisaikolojia, wakiona vurugu, matusi, na ugomvi wa mara kwa mara.
“Watoto wanaoishi katika nyumba zinazouza pombe mara nyingi huathirika kimwili, kisaikolojia na hata kielimu. Wanakosa mazingira salama ya kukua, wanashuhudia vitendo vya unyanyasaji, na wakati mwingine wao wenyewe wanakumbana na ukatili,” anasema.
Wataalamu wa afya na jamii wanasema pombe ina madhara makubwa kwa jamii, hasa inapokuwa katika mazingira yasiyodhibitiwa.
Daktari wa Saikolojia, Dk. John Lugenge, anasema watoto wanaokulia kwenye nyumba zinazouza pombe wanakabiliwa na msongo wa mawazo, woga, na wakati mwingine huiga tabia za walevi.
Katika kata ya Kalenga na sehemu nyingine nchini Tanzania, Laurent anasema pombe inabaki kuwa changamoto kubwa kwa ustawi wa watoto.

“Udhibiti dhaifu wa uuzaji wa pombe, na mazingira yasiyo salama yanawaweka watoto katika hatari kubwa ya ukatili na madhara ya kiafya,” anasema.
Mjadala huo kwa mujibu wa mwanasheria Baraka Kimata wa mjini Iringa unafichua mgongano mkubwa wa kisheria na kijamii.
Wakati Sheria za Tanzania zinaruhusu vijana wa miaka 15 kuanza kutumia pombe, wazalishaji wa vileo wanakataza kuuza kwa walio chini ya miaka 18.
Zaidi ya hayo, Sheria ya Mtoto ya 2009 inasisitiza ulinzi wa watoto dhidi ya tabia hatarishi, huku sheria nyingine ikiruhusu pombe kuuzwa katika maeneo yasiyo salama kwao.
Katika mazingira haya yenye utata, anasema kuna mgongano wa Sheria Kuhusu Pombe kwa Watoto.
“Sheria ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe ya mwaka 1968 inaruhusu vijana wa miaka 15 kuanza kutumia pombe, lakini Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 inamtambua mtu chini ya miaka 18 kama mtoto anayepaswa kulindwa dhidi ya tabia hatarishi,” anasema
Mratibu wa Kinga ya Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Goodluck Tumaini, anakiri kuwa sheria ya pombe ni ya zamani na inahitaji kufanyiwa marekebisho.
Anaeleza kuwa sheria hiyo inaruhusu utoaji wa leseni mbalimbali za kuuza pombe, lakini utekelezaji wake umekuwa dhaifu.
Katika uhalisia wa sasa, baa zimekuwa zikifunguliwa bila kuzingatia masharti ya umbali wa kilometa moja kutoka baa moja hadi nyingine. Badala yake, baadhi ya mitaa zina baa zinazofuatana, hali inayowafanya watoto waishi na kushuhudia unywaji wa pombe kila siku.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omari Ubuguyu, , Tanzania ni nchi ya tatu kwa unywaji wa pombe barani Afrika.
Kiwango cha unywaji wa pombe kimezidi hata baadhi ya nchi za Ulaya huku vijana wa miaka 15 na kuendelea wakitumia lita 10.4 kwa mwaka – kiwango kikubwa kinachohatarisha afya zao.
Hata hivyo serikali kwa kupitia vyanzo vyake mbalimbali inasema inatambua tatizo la matumizi mabaya ya pombe na imekuwa ikijadili mabadiliko ya sheria ili kuhakikisha watoto wanalindwa ipasavyo.
Hata hivyo pamoja na utambuzi huo, wadau mbalimbali wanasema utekelezaji wa sheria zilizopo bado unasuasua, huku changamoto kuu zikiwa ni pamoja na udhibiti dhaifu wa maeneo ya uuzaji pombe.
Elimu finyu kuhusu madhara ya pombe – Wazazi wengi hawana uelewa wa kina kuhusu athari za pombe kwa watoto, na baadhi yao huwaruhusu au hata kuwashawishi watoto wao kuanza kutumia vileo.
Ukosefu wa sera madhubuti za utekelezaji wa sheria – Ingawa sheria inasema watoto wasiruhusiwe kuingia katika maeneo ya uuzaji pombe, bado kuna baa nyingi ambapo watoto wanahudhuria kama wateja au hata wafanyakazi.
Wanasema Tanzania inapaswa kuchukua hatua madhubuti – kudhibiti kwa ukali uuzaji wa pombe, kuimarisha elimu kwa jamii, na kuboresha na kutekeleza sheria ipasavyo ili kupunguza kiwango cha unywaji wa pombe kwa watoto na kupunguza visa vya ukatili unaotokana na pombe.
Bila hatua madhubuti, watoto wa Kalenga na Tanzania kwa ujumla wataendelea kuathirika kutokana na mfumo usio na uwazi kuhusu matumizi ya pombe, na athari zake kwa maisha yao zitabaki kuwa mzigo wa kizazi kijacho.



