Posho, mishahara ya wabunge ikatwe – Kunti

DODOMA; MBUNGE wa Viti Maalum, Kunti Majala amependekeza kwa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuwa wabunge wasilipwe posho za vikao na mishahara ya mwezi huu ili waonje uchungu wanaokutana nao Watanzania ambao hawajalipwa mafao yao ya kustaafu.

Ameyasema hayo leo Novemba 4, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji ya Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2022.

Amesema, watumishi wanadai Sh bilioni 119 na kwamba anajiuliza kama kuna mbunge anayedai serikali hata Sh 100.

“Watumishi wanadai malipo ya muda mrefu mfano wa Halmashauri ya Chemba ambayo ina watumishi 79 wanaodai tangu wako katika halmashauri ya Kondoa,” amesema na kuongeza
“Kama sio kikao hiki basi kikao kijacho na sisi usitulipe mshahara na posho za bunge lijalo…usitulipe ili tuonje uchungu huu ambao wanakumbana nao Watanzania wenzetu waliolitumikia Taifa hili, pamoja na wazee wastaafu ambao wamelitumikia Taifa hili,” amesema.

Ameitaka Serikali kuwalipa watumishi wastaafu wanaodai malipo yao.

Hoja ya mbunge huyo ilimfanya Spika kuwahoji wabunge kama wanaafikiana na kile kilichopendekezwa, hata hivyo ilisikika minong’ono ya chini na ndipo Dk Tulia akasema kuwa ni mbunge mmoja aliunga mkono kwa hivyo ni wachache.

Naye Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Kilumbe Ng’enda alimpa taarifa Kunti kuwa jukumu la kuwalipa wafanyakazi wasiolipwa, lipo mikononi mwa Serikali hivyo akapendekeza kuwa mawaziri ndiyo wanaotakiwa kuzuiliwa mishahara yao.

Akiendelea kuchangia, Kunti amesema amefanya hivyo kwa sababu alitaka kuona ni kwa namna gani mawaziri wanaweza kunyoosha mkono kwa makosa yao ya kushindwa kuwasimamia watendaji wao.

“Umeona uzalendo wa mawaziri wetu, kosa wamefanya wao la kushindwa kuwasimamia watumishi wao, wanashindwa kunyoosha mkono kwa makosa ambayo wameshindwa kuwasimamia watu wao,” amesema.

Amewataka kutimiza majukumu yao na kwamba mawaziri wana magari ya kutembelea lakini watumishi wanatembea kwa miguu.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button