PPAA inavyotumia 4R kuimarisha uwazi ununuzi wa umma

NI miaka minne na mwezi mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani chini ya uongozi imara na thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia aliingia madarakani Machi 19, 2021 na wakati wote wa uongozi wake, serikali imekuwa ikisisitiza na kusimamia uwazi na uwajibikaji katika sekta ya ununuzi wa umma kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa tija na kuwaletea wananchi maendeleo kwa wakati uliokusudiwa.
Watanzania wakiwa wanaadhimisha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, makala haya yanaangazia mafanikio katika taasisi zinazosimamia sekta ya ununuzi wa umma ambayo ni Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA).
Kwa mujibu wa sheria hiyo, jukumu kuu la PPAA ni kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi ya malalamiko au rufaa zitokanazo na maamuzi ya maofisa masuuli wa taasisi za umma katika michakato ya ununuzi wa umma. Aidha, inapokea na kusikiliza malalamiko ya wazabuni ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa kufungiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi imara wa Rais Samia imeendelea kudumisha misingi ya utawala bora ikiwemo haki na usawa, pamoja na kuendelea kusimamia miradi ya kimkakati yenye tija kwa nchi na hivyo kuiwezesha serikali kupata thamani halisi ya fedha katika ununuzi wa umma.
Ikiwa takribani asilimia 70 ya bajeti ya serikali hutumika kwa ajili ya ununuzi wa umma, sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi wa umma zinaiwezesha serikali kuendelea kuimarisha sekta ya ununuzi.
Katika kipindi cha uongozi wa Rais Samia, PPAA imeendelea kutekeleza jukumu lake kuu la utatuzi wa migogoro itokanayo na michakato ya ununuzi wa umma kwa haki, uwazi, uadilifu na kwa muda mfupi.
Haya yote yanalenga kuwezesha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha na kufikia malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati. PPAA chini ya uongozi imara wa Rais Samia imefanikiwa kutekeleza majukumu yake katika maeneo ya falsafa ya R Nne (4R) za Rais Samia.
‘Reconciliation’ yaani Maridhiano
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, PPAA imeshughulikia mashauri 171 yaliyotokana na michakato ya ununuzi wa umma. Katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 36 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika.
Hatua hiyo iliepusha utekelezaji usioridhisha wa miradi unaosababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi. Serikali ya Awamu ya Sita inaamini kuwa, usuluhishi wa migogoro hauwezi
kupatikana penye ubaguzi na mahali ambapo kuna wanaokosa fursa na haki zao za kiuchumi na kiraia.
Kitendo cha PPAA kuzuia utoaji wa tuzo kwa wazabuni 36 waliokosa sifa kinaweka uzito katika usuluhishi wa migogoro ambayo ni falsafa ya Rais Samia. PPAA pia imeendelea kudhibiti taasisi nunuzi kukiuka taratibu za kisheria hasa katika tathmini ya zabuni katika baadhi ya mashauri.
Mamlaka pia imefanikiwa kubaini ukiukwaji wa taratibu za kufanya tathmini uliofanywa na taasisi nunuzi ikiwemo kutozingatia vigezo vilivyowekwa katika kabrasha la zabuni au kuongeza vigezo vipya ambavyo havikuwepo awali.
‘Reform’ yaani Mageuzi
Katika kipindi hicho chini ya Rais Samia, Serikali imewezesha kutungwa upya kwa Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023 na kuruhusu hatua za mageuzi kuchukuliwa ilipobainika kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu katika mchakato wa ununuzi.
Kupitia sheria mpya ya ununuzi wa umma, mageuzi yaliyofanyika ni pamoja na kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko au rufaa zinazotokana na michakato ya ununuzi wa umma. Mfano katika hilo ni kupunguzwa muda wa siku saba za kazi kwa ajili ya kusubiri malalamiko ya wazabuni kabla ya kutoa tuzo na kuwa siku tano za kazi.
Muda huo hautajumuisha njia za ununuzi ambazo hazihitaji ushindani ambazo ni ununuzi kwa mzabuni mmoja, ununuzi mdogo na ununuzi wa duka moja kwa moja.
Muda wa ofisa masuuli kushughulikia malalamiko ya zabuni pia umepunguzwa kutoka siku saba za kazi hadi siku tano za kazi na pale ofisa huyo atakapounda jopo la mapitio ya malalamiko atatumia siku saba za kazi kushughulikia na atatakiwa kuwajulisha washiriki wa zabuni kuwepo kwa jopo na muda wa PPAA kushughulikia malalamiko au rufaa kutoka siku 45 hadi siku 40.
Mageuzi mengine ni kuweka masharti ya lazima kwa taasisi nunuzi kufanya ununuzi kupitia mfumo wa kieletroniki. Katika hilo, PPAA imefanikiwa kuanzisha moduli mpya ya kuwasilisha rufaa/ malalamiko kwa njia ya kieletroniki inayorahisisha uwasilishaji wa malalamiko na kutoa fursa kwa wazabuni wengi zaidi kuwasilisha malalamiko yao.
Moduli hiyo ni rafiki na inaokoa muda wa kuwasilisha malalamiko. Moduli hiyo imewekwa kwenye Mfumo wa Ununuzi wa Umma Kieletroniki (NeST) uliojengwa chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.
Ili kuwezesha matumizi ya moduli kwa ufasaha, PPAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ilitoa mafunzo kwa washiriki kutoka katika taasisi nunuzi na wazabuni takribani 913 wa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na Pwani yaliyofanyika Dar es Salaam, Mei 2024.
Katika Kanda ya Ziwa yaani mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara, Geita na Simiyu, mafunzo hayo yalifanyika Februari, 2025 jijini Mwanza yakiwahusisha maofisa ununuzi, wakuu wa vitengo vya ununuzi, wakuu wa vitengo vya sheria, maofisa sheria, maofisa Tehama, mawakili na wazabuni.
Matumizi ya (Tehama) Moduli ya Kieletroniki
Februari, 2025 Serikali kupitia Wizara ya Fedha ilizindua rasmi matumizi ya moduli ya kupokea na kushughulikia malalamiko na rufaa katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya Kieletroniki (NeST) jijini Mwanza kwa wazabuni na taasisi nunuzi za Mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara, Geita na Simiyu.
Katika Hotuba yake, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba iliyosomwa na Kamishna wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Dk Fredrick Mwakibinga, anasema kuanza kwa matumizi ya moduli kuna faida nyingi zikiwemo za kuokoa muda na gharama zilizokuwa zikiingiwa wakati wa uwasilishaji wa rufaa na majibu ya hoja za rufaa, kupunguza mianya ya rushwa, pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika ununuzi wa umma.
Faida nyingine ni pamoja na kuwawezesha wahusika katika shauri kufuatilia na kufahamu hatua zote za
uchakataji wa shauri linaloendelea.
Mengine ni kutungwa kwa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma Katika Kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Fedha, imeiwezesha PPAA kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi zinazosimamia ununuzi wa umma nchini, kuandaa Kanuni za Rufaa za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2024 zilizotangazwa Januari 31, 2025 kupitia Gazeti la Serikali (GN No.65/2025).
‘Rebuilding’ yaani Ujenzi mpya
Serikali ya Awamu ya Sita imewezesha na kuboresha usimamizi wa sekta ya ununuzi wa umma nchini. Hatua hiyo imeiwezesha PPAA kuwajengea uwezo wajumbe wa mamlaka na watumishi wake na kuboresha mazingira ya kazi kwa kuwapa vifaa muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya PPAA na kuiwezesha serikali kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa wakati.
‘Resilience’ yaani Ustahimilivu
Licha ya athari za kiuchumi zilizoikumba na zinazoendelea kuikumba dunia na kutikisa uchumi zilikiwa zilizotokana na ugonjwa wa Uviko 19, vita baina ya Urusi na Ukraine pamoja na kuadimika kwa fedha za kigeni, Serikali ya Tanzania imeendelea kuiwezesha PPAA kustahimili athari hizo na kutekeleza majukumu yake ipasavyo.