PPRA yafafanua NeST ilivyonufaisha vikundi 210

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imesema tangu kuanza kwa matumizi ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) Julai 1, 2023 hadi Oktoba 8, 2024, jumla ya vikundi 210 vimefanikiwa kupata tuzo za zabuni zenye jumla ya thamani ya zaidi ya Sh bilioni 9.
 
Aidha mamlaka hiyo imefafanua kuwa mwaka wa fedha uliopita, kuanzia Julai 1, 2023 hadi Juni 30, 2024, vikundi 85 vya vijana vimepata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.9.
 
Akizungumza leo Novemba 4, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba amebainisha kuwa mbali na hayo pia tangu Julai 1, 2023 hadi Juni 30, 2024, vikundi 84 vya wanawake vimefanikiwa kupata zabuni zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 4 na vikundi viwili vya wazee vimepata zabuni zenye thamani ya Sh milioni 78.
 
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF, Deodatus Balile ameipongeza PPRA kwa kuja na mfumo wa NeST kwani umewarahisisha watanzania kushiriki Katika zabuni za manunuzi ya umma huku akiongeza kuwa wapotayari kutumia vyombo vya habari kuuelezea mfumo huo kwa wananchi Ili zabuni nyingi za manunuzi ya uuma ziweze kufanywa watanzania.
 
Hadi sasa PPRA kupitia mfumo wake wa NeST imeweza kusajili wazabuni zaidi ya 28,000 huku mikataba ya zabuni 62,267 yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 10.2 ikiwa imetolewa kwa wazabuni kupitia mfumo huo.