Prof Bisanda asisitiza utunzaji rasimali Chuo Kikuu huria

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda amesisitiza utunzaji sahihi wa rasilimali za chuo hicho yakiwemo magari manne aina ya Toyota Hillux “Double Cabin” yaliyonunuliwa kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) chuoni hapo.

Amesema magari hayo yakitunzwa vizuri yatadumu na kusaidia chuo hicho kutimiza malengo yaliyokusudiwa.

“Katika kipindi cha hivi karibuni, serikali imekuwa ikituangalia kwa karibu sana. Bado tuna majengo saba ya maabara za kikanda yatakayoanza kujengwa hivi karibuni chini ya Mradi wa HEET halikadhalika serikali kupitia fedha za maendeleo inajenga Kituo cha Uratibu cha Pemba,” amesema.

Ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya chuo hicho ili kiweze kuwa karibu zaidi na jamii na kushiriki moja kwa moja katika kuleta maendeleo nchini.

Prof Bisanda amewakumbusha watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha malengo ya utekelezaji wa mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho, anayesimamia Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri wa Kitaalam, Profesa Alex Makulilo amesema magari hayo yatatumika kusaidia shughuli za utekelezaji wa Mradi wa HEET wa maabara za sayansi katika mikoa ya Arusha, Kigoma, Mtwara, Mwanza, Morogoro, Pwani na Njombe.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Huduma za Mikoa na Teknolojia za Kujifunzia, Profesa Leonard Fweja amewataka watumishi wote kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kuijengea serikali imani kwa Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania ili iendelee kuwekeza miradi mbalimbali katika chuo hicho.

Habari Zifananazo

Back to top button