Prof. Bisanda: Umri si kikwazo cha elimu

WATANZANIA wametakiwa kuondoa dhana ya kwamba umri ukisogea basi hakuna tena fursa ya kujiendeleza elimu ya juu.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Profesa Elifas Bisanda amesema hayo alipotembelea banda la maonesho la chuo hicho katika maonesho ya pili ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) yanayoendelea  jijini Arusha.

Profesa Bisanda amesema dhana ya mtu kusema ukiwa mzee huwezi tena kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu kwa sasa imepitwa na wakati, kwani OUT inatoa fursa kwa marika yote bila kubagua umri na shughuli zao.

“Shughuli haziwezi kufa au kusimama kwa sababu zozote za kishule, kwani wanasoma huku wakiendelea na shughuli zao za kila siku,” amesema Profesa Bisanda.

Makamu Mkuu wa OUT, Profesa Elifas Bisanda

Amesema kinachoangaliwa katika kujiunga na chuo hicho ni ukamilifu wa vigezo vinavyotakiwa katika kujiunga na elimu ya juu pekee, kwani kwa mfumo wa elimu wanayoitoa hata asiyeweza kujongea anaweza kumudu kusoma.

Kwa upande wake mwanafunzi wa chuo hicho  anayesoma programu ya msingi,  Felix Ringo (55),  amesema amejiunga OUT kwa dhamira ya kufika mbali kitaaluma.

“Kwa umri huu nilionao nimebanwa na mambo mengi nisingeweza kujiendeleza kupitia elimu za kukaa darasani, kupitia Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, nimepata fursa adhimu kabisa na nina shauku kubwa ya kusoma hadi kufikia ngazi za juu za usomi. Nimeanza mwaka huu na ninajiandaa na mitihani ya majaribio hivi karibuni,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Masoko, Dk Mohamed Maguo, amesema dhima halisi ya uanzishwaji wa chuo hicho ilikuwa ni kuwainua kielimu watumishi na watu waliokosa fursa ya kuhudhuria elimu za darasani kutokana na kubanwa na majukumu mbalimbali ya kimaisha.

“Hivyo hata wale wanaohisi umri wao umeanza kuwatupa mkono, chuo hiki ni sehemu pekee yenye fursa ya wao kupata elimu ya juu ambayo wanahisi walishaipoteza,” amesema.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x