‘PSSSF imeanza kulipa mafao kikokotoo kilichoboreshwa’

DAR ES SALAAM; MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umeanza kutekeelza maagizo ya serikali ya kuanza kulipa Mafao kwa kutumia utaratibu wa kikokotoo kilichoboreshwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ametangaza.

Waziri Kikwete ametangaza hayo leo Novemba 20, 2024 jijini Dar es salaam, mbele ya wastaafu watarajiwa wanaochangia PSSSF, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuishi baada ya kustaafu.

“Serikali ya Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan, ilisikia kilio cha wastaafu, na leo hii ninapenda kutangaza rasmi  kwamba  hadi kufikia jana (Novemba 19, 2024), jumla ya wastaafu 10,414 ambao wamestaafu kuanzia Julai 2022 na kuanza kulipwa kwa kutumia kikokotoo kile kilicholeta taharuki wameshalipwa mapunjo na kazi bado inaendelea,” amesema Waziri Kikwete na kuongeza:

Advertisement

“Lakini jumla ya wastaafu wapya  2,479  ambao wamestaafu kuanzia Julai 1, 2024 wameshalipwa mafao yao kwa kutumia kikokotoo kipya kilichoboreshwa na kazi bado inaendelea.”

Amesema serikali imeridhia maboresho yafuatayo yafanyike kuanzia mwezi Januari 2025, ambayo ni pamoja na wastaafu ambao wengi wamekuwa wakipokea kile kima cha chini cha kiasi cha Sh 100,000. sasa kuanzia pensheni ya Januari 2025 pensheni yao ya mwezi itaongezeka kutoka shilingi 100,000 hadi shilingi 150,000.

Baadhi ya wastaafu watarajiwa wa PSSSF,wakifatilia hotuba ya Waziri Ridhiwani Kikwete

Amesema wastaafu ambao walikua wakipokea pensheni ambayo ni zaidi ya Sh 150,000.00 na wao watapewa ongezeka la asilimia 2 kila mmoja.

Katika maboresho hayo, pia mstaafu yeyote anayepokea pensheni katika Mfuko wa PSSSF akifariki, Mfuko utatoa kiasi cha Sh 500,000.00 kwa ajili ya maziko (funeral grant), huku Mstaafu yoyote akifariki wategemezi wake wanaotambulika na sheria ya Mfuko watalipwa mkupuo wa miezi 36 wa pensheni ya mwezi ya mstaafu husika.

Soma pia:‘Tutaendelea kuelimisha kanuni mpya ya kikokotoo

“Utaratibu huu ulishaanza tangu Julai 2022 lakini ulikuwa unatumika kwa wastaafu waliokuwa wanalipwa kwa kikokotoo kipya, lakini sasa utaratibu huu unafunguliwa kwa wastaafu wote hadi wale waliolipwa kwakutumia vikokotoo vya zamani vya kwenye mifuko iliyounganishwa,” amefafanua Waziri Kikwete.

Amewahakikishia wastaafu kuwa ustahamilivu wa Mfukoa PSSSF umeendelea kuimarika kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia 36.4 hivi sasa.

Akimkaribisha Waziri Kikwete kutoa hotuba yake, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Abdul-Razaq Badru, amesema, tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa PSSSF tayari umelipa jumla ya mafao yenye kiasi cha shilingi trilioni 10.46 kwa wanufaika 310,458.

“Kwa kiasi hiki kilicholipwa ndani ya miaka sita ya Mfuko, kinaonesha haja ya kuandaa mpango wa mafunzo maalumu kwa ajili ya Wanachama wake wanaotarajia kustaafu ndani ya kipindi cha miaka miwili; Mafunzo haya yatalenga maeneo ya uwekezaji katika viwanda vidogo vidogo na vya kati, uwekezaji katika masoko ya fedha, kilimo biashara na ujasiriamali kwa ujumla,” amesema.